Wiki moja au siku saba kati ya Juni 27, 2013 na Julai 4, 2013 Tanzania itapata ugeni mzito unaoweza kubadili historia ya nchi hii. Rais wa Marekani Barrack Obama anatarajiwa kuwa mmoja wa wageni watakaofika hapa nchini, kwa nia ya kuendeleza uhusiano kati ya Tanzania na Marekani.

Kabla ya Rais Obama, Julai 27, 2013 Rais wa Sri Lanka, Mahinda Rajapaksa, anatarajiwa kufika nchini siku hiyo kwa ajili ya ziara ya kitaifa. Kati ya mambo anayotarajiwa kufanya Rais huyu, ni pamoja na kusaini mikataba mitatu ikiwamo ushirikiano wa kiuchumi, mkataba wa utalii na ule wa kutotozwa kodi mara mbili.

 

Hii ni ziara ya kihistoria baada ya Sri Lanka, nchi iliyokuwa na vita miaka 30 kurejea katika utulivu na amani. Habari za uhakika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, zinasema Novemba mwaka huu, Sri Lanka itakuwa mwenyekiti wa Mkutano wa Jumuiya ya Madola, kwa maana kuwa Rais huyu atakuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madola.

 

Ukiacha hilo, Rais Rajapaksa atakuwa mmoja kati ya marais 16 wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano wa Smart Partnership unaotarajiwa kufanyika kwa mara ya kwanza hapa nchini. “Hii ni historia. Inadhihirisha kazi nzuri ya uhusiano wa kimataifa aliyoifanya Rais Jakaya Kikwete. Hakuna nchi yoyote iliyopata kuwa na mkutano wa Smart Partnership ikapata marais 16. Tanzania imevunja rekodi,” alisema mtoa habari wetu.

 

Nchi ambazo zimethibitisha marais wake kuhudhuria ni pamoja na Benin, Gabon, Sudan Kusini, Namibia, Comoro, Zimbabwe, Swaziland, Malaysia, Lesotho, Botswana, Zambia na nyinginezo. Mkutano huu utafanyika kati ya Julai 28, 29 na 30, mwaka huu.

 

Julai 1, 2013 anawasili nchini Rais Obama. Huu ni ugeni wenye mvuto wa pekee. Rais Obama anakuja hapa nchini kuimarisha uhusiano kati ya Marekani na Tanzania.

 

“Kimsingi uhusiano wa Marekani na Tanzania umekua zaidi katika miaka 10 iliyopita kuliko wakati wowote,” alisema mtoa habari wetu.

 

Marekani inaisaidia Tanzania katika maeneo ya afya, miundombinu kama umeme, maji, barabara na kilimo, maeneo yanayoaminika kuwa yanaweza kuwasaidia wananchi kujitegemea kiuchumi. Ufadhili wa Marekani unapitia kwenye mradi wa Millennium Challenge Corporation (MCC).

 

Tanzania imefanya vyema katika mradi wa kwanza wa MCC ambapo nchi ilipata wastani wa dola milioni 698. Mwaka 2001  karibu Sh bilioni 1,116,800 kama msaada kutoka Marekani.

Baada ya Tanzania kuthibitika kuwa imezitumia vizuri fedha za MCC I, sasa Rais Obama anatarajiwa kuzindua awamu ya pili ya mradi wa MCC itakayolipatia taifa la Tanzania mabilioni ya shilingi.

 

Zipo fursa za kibiashara ambazo Tanzania inaweza kuzipata kwa kuziendeleza chini ya uhusiano huu kama mikataba ya AGOA inayowaruhusu wafanyabiashara kutoka Tanzania kuuza bidhaa na huduma nchini Marekani kwa masharti nafuu.

 

Katika hali ambayo haikutarajiwa na wengi, taarifa za uhakika zinasema Obama atakuja na mke wake, Michelle na watoto wake wawili – Maria na Shasa.

 

Rais Obama, kwa mujibu wa taarifa za awali, anapaswa kukaa hapa nchini hadi Julai 2, atakapoondoka.

 

Kwa neema ya aina yake, siku ya Julai 2, 2013 Rais mstaafu wa Marekani, George W. Bush na mkewe, Laura Bush, watatua hapa nchini pia.

 

Bush na mkewe watashiriki tukio kubwa la mkutano wa wake za marais wote barani Afrika, watakaokuwa hapa nchini kujadili ajenda ya Kumwezesha Mwanamke na Afya.

 

Mkutano huu unaotarajiwa kuanza Julai 3, nao unaelezwa kuwa mmoja wa mikutano mkubwa kupata kutokea barani Afrika, ambapo wake za marais wote 54 za Afrika watakuwa hapa nchini kushiriki mkutano huo wa aina yake.

 

Kama hiyo haitoshi, Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, naye atakuja hapa nchini Julai 2, kwa nia ya kushiriki mkutano wa Kamisheni ya Marais wa Afrika Kusini na Tanzania ambapo atakaa hadi ufunguzi rasmi wa maonesho ya Sabasaba atakapokuwa mgeni rasmi.

 

Ugeni huu ni wa aina yake kupata kutokea hapa nchini ndani ya muda wa wiki moja. Wachambuzi wa mambo wanasema ugeni huu umetokana na uwezo na ushirikiano mzuri alionao Rais Jakaya Kikwete na jamii ya kimataifa.

 

Wengi wanasema ikiwa ugeni huu utashikiliwa vyema utakuwa wenye manufaa kwa taifa letu kiuchumi, kijamii na kiutalii.  “Hawa wageni wote wakija, wenye baa watauza, wenye hoteli watauza, na kila mtu atatengeneza fedha. Ombi ni moja tu, tuwaheshimu wageni hawa, tuwapende na kuwaonesha ukarimu. Tusiwatendee matendo yatakayowasononesha,” alisema mtoa habari wetu.