Wiki iliyopita yamekuwapo matukio mengi, lakini kwa ngazi ya Bara la Afrika yaliyotawala ni vurugu za xenophobia nchini Afrika Kusini na kifo cha Baba wa Taifa la Zimbabwe, Robert Mugabe.
Wageni kadhaa wanaofanya biashara zao nchini Afrika Kusini, hasa katika miji ya Johannesburg na Pretoria, wameuawa na wengine kujeruhiwa kwa kile kinachoonekana ni chuki ya wenyeji dhidi ya wageni. Mali za mabilioni ya fedha zimechomwa moto na nyingine zimeporwa.
Miongoni mwa sababu za vurugu hizo ni kilio cha vijana wa Afrika Kusini cha kazi zao kupokwa na wageni. Hili linahitaji mjadala, kwa sababu yapo maelezo kuwa vijana wengi katika nchi hiyo wamebweteka, hawajitumi kufanya kazi, kwa hiyo wageni wametumia mwanya huo kuendesha biashara.
Kwa Tanzania tuna la kujifunza. Vijana wetu wasimalizie akili kwenye kamari tu, bali wajielekeze kwenye uzalishaji ili wasije kugutuka na kukuta maeneo yote ya uchumi yamekamatwa na wageni.
Pamoja na yote yanayoendelea Afrika Kusini, tunalaani kwa nguvu zote mauaji na vitendo vya uhalifu dhidi ya binadamu, tena wa bara moja.
Pili, tunaungana na Wazimbabwe na dunia ya wanamajumui wote katika kuomboleza kifo cha Komredi Mugabe.
Mzee Mugabe hakuwa malaika. Alikuwa na udhaifu wake kama binadamu, lakini kwenye mizania jina lake litabaki kuwa alama kati ya alama chache za Waafrika wachache waliojitolea kwa hali zao zote kupigania heshima na uhuru wa mtu mweusi.
Mzee Mugabe alishiriki mapambano ya kuikomboa Zimbabwe mwaka 1980, pia alikuwa miongoni mwa miamba ya Afrika iliyoshiriki katika harakati za kuhakikisha ukoloni unatokomezwa katika mataifa ya Namibia na Afrika Kusini.
Chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mzee Mugabe alishirikiana na viongozi wengine katika kusimama imara kutetea utu wa Mwafrika dhidi ya uonevu wa makaburu na vibaraka wao, lakini pia na mataifa makubwa ya magharibi.
Bila woga, alikuwa mstari wa mbele kuyasema mataifa makubwa kwa vitendo vyao vya ukandamizaji, bila kusahau suala la ardhi nchini mwake iliyohodhiwa na wachache. Asilimia 90 ya ardhi nzuri nchini Zimbabwe inahodhiwa na Wazungu ambao ni asilimia 3 pekee ya watu wote.
Hatua ya Mugabe kupigania ardhi iliwaudhi ‘wakubwa’ hata wakaamua kumwekea vikwazo vya kiuchumi na kumzuia kusafiri katika mataifa yao. Hakuteteleka.
Tunawapa pole Wazimbabwe na kutoa mwito kwa kizazi cha sasa cha Afrika kutambua na kuenzi kazi za mashujaa kama Robert Mugabe.