NA Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha
Kuelekea katika wiki ya AZAKI, Mkurugenzi Mtendaji wa FCS Justice Rutenge amewahimiza wananchi kupaza sauti zao kwa kutoa maoni yatakayopelekea kupata dira bora kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Rutenge amesema hayo Dar es Saalam wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI) 2025, ambapo zaidi ya washiriki 500 wanatarajiwa kushiriki na kutoa wito kwa watanzania kushiriki kwa wingi.

“Wiki ya Azaki imefanyika kwa miaka sita mfululizo na sasa ni mwaka wa Saba lengo likiwa kuwaleta pamoja wadau wa sekta ya Azaki kufanya mijadala mbalimbali ya maendeleo kwa mustakabali wa nchi yetu Tanzania,
“Kila mwaka tuna utaratibu wa kuangazia mambo mbalimbali na kuweka sawa Mahudhui ya wiki ya Azaki na mwaka huu tutaangazia mchakato mzima wa dira ya Taifa.
“Watanzania wengi wanatambua kuwa mwaka huu tumeshiriki kwa kina kwenye mchakato wa kutengeneza dira yetu ya maendeleo ya mwaka 2050 ambayo ni fursa inayokujaga mara chache mara moja kwa miongo miwili au miwili na nusu.

Kwa upande wake Mkurugenzi mkazi, CBM International ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati za Asasi za Kiraia Nesia Mahenge amesema wiki hiyo inalenga kutatua changamoto ambazo zipo katika azaki za kiraia na kuona ni namna gani zinatatuliwa.
“Azaki kutoka nchi za Tanzania bara, Zanzibar wanaangalia ni namna gani kila mwaka ndani ya wiki moja tunakutana na kutathimini kazi za mashirika yasio ya kiserikali kuangalia maendeleo ambayo tumeyaleta katika nchi yetu.
“Kwa mwaka huu itakuwa tofauti tulizoea kufanya mwezi wa kumi mkoani Dodoma lakini kwa sasa ni Arusha kutokana na mapendekezo ya jamii hatutafanya mkoa mmoja.
“Tujumuike kuangalia jinsi ya kupanga mikakati na kutenga fedha za kuleta maendeleo kwenye jamii na pia mataifa mengine kuangalia maendeleo yetu na kuyapeleka kwenye nchi zao.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkaazi wa Trademark Africa Elibariki Shami, amesema kuwa FCS imeonesha jitiaha kubwa katika kuimarisha utetezi wa AZAKi kwa kuhakikisha haki za walaji zinapatikana na kuongeza uelewa katika ulinzi wa watumiaji.
“FCS inalenga kuhakikisha kuwa ifikapo 2026, AZAKi zinashiriki kikamilifu katika mipango ya ulinzi wa watumiaji na kuwepo kwa ongezeko la uelewa wa jamii juu ya ulinzi wa walaji” amesema.
Ameongeza kuwa kushiriki wa moja kwa moja wa FCS katika kushughulikia masuala ya kijamii, sambamba na utaalamu wa utetezi na kujitolea, unawakilisha maslahi ya raia na walaji, nakwamba AZAKi huziba pengo kati ya sera na hatua za msingi za kuhakikisha ulinzi thabiti wa walaji unakuwepo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Association NGoS Adamsoni Nsimba amesema wamefurahi kujumuika katika uzinduzi wa wiki za Azaki itakayomsaidia na kumlinda mlaji na kujenga uwezo kwa jamii na kumpa mlaji haki tofauti na mfanya biashara kuchagiza sera na sheria.

