Takwimu za Jeshi la Polisi na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusiana na  vifo vinavyosababishwa na matukio ya ajali za  barabarani Tanzania zimezua hofu ya mwenendo halisi wa usalama barabarani nchini.

Desemba mwaka jana, shirika hilo limetoa ripoti yake ijulikanayo kama ‘Global status report on road safety 2018’, imebainisha kwamba matukio yaliyosababisha vifo kutokana na ajali za barabarani na kuripotiwa na Jeshi la Polisi kwa mwaka 2016 ni 3,256, tofauti na uchambuzi kwenye ripoti hiyo unaoonyesha kuwa ni makisio ya matukio 16,252.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya WHO, nakisi ya takwimu kati ya mamlaka hizo mbili ni 13,006, ukweli unaoibua sintofahamu na mkanganyiko wa hali na mwenendo halisi wa usalama barabarani nchini.

Hivyo, ripoti kama hiyo ya WHO ya mwaka 2015  nayo inasema matukio yaliyoripotiwa na Jeshi la Polisi kwa mwaka 2013 ni 4,002, tofauti na uchunguzi kwenye ripoti hiyo unaoonyesha ni makisio ya matukio ya vifo 16,211. Nakisi kwa mwaka huo nayo ni kubwa, 12,209.

Ripoti zote zimeyataja makundi ya watembea kwa miguu pamoja na kundi la abiria na madereva wa magari makubwa na madogo kuwa ndiyo makundi yanayoathirika zaidi kwenye ajali za barabarani kwa kuwa na wastani wa asilimia 30 ya vifo.

Ripoti ya mwaka jana inasema kundi la watembea kwa miguu ndilo lililoongoza kwa asilimia 31 ya vifo vitokanavyo na ajali za barabarani likifuatiwa na kundi la abiria na madereva wa magari makubwa na madogo kwa asilimia 28.

Kundi jingine linaloonekana kuathirika kutokana na ajali hizo ni madereva wa pikipiki na Bajaj kwani idadi inaonekana kuongezeka kutoka asilimia 22 kwa mujibu wa ripoti ya WHO ya mwaka 2015 hadi asilimia 23 mwaka jana.

Tanzania kama zilivyo nchi nyingine zenye uchumi mdogo duniani, zinatajwa katika ripoti hiyo kuwa hazina jitihada za kupunguza idadi ya ajali zinazosababisha vifo na majeruhi huku zikiwa na idadi kubwa ya ajali mara tatu zaidi ikilinganishwa na nchi zilizoendelea.

Akizungumza na JAMHURI, Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Muslim, amekanusha takwimu hizo zilizotolewa na WHO na kusema kuwa kwa sasa ajali za barabarani zinaendelea kupungua kwa kiasi kikubwa.

Amesema sheria inasema suala la takwimu za usalama barabarani zinapaswa kutolewa na Jeshi la Polisi pekee na si mamlaka nyingine, na kwamba utofauti huo unatokana na WHO kuchukua takwimu hizo kutoka vyanzo visivyo na mamlaka na utaalamu wa masuala ya ukusanyaji wa taarifa za ajali za barabarani.

Kamanda Muslim amesema kwa sasa madereva wengi wameanza kutii sheria za usalama barabarani na kutaja sababu zilizochangia kupunguza ajali za barabarani kuwa ni operesheni yake ya ‘Nyakua nyakua’ pamoja na kuwepo kwa tochi za barabarani.

“Anayesema ajali zinaongezeka atakuwa na masilahi yake upande fulani, hata ukienda hospitalini katika wodi za majeruhi kama vile MOI utakuwa shahidi mzuri wa ajali za barabarani.

“Lakini mfano mzuri ni kipindi cha sikukuu mwaka jana, hakuna ajali kama tulivyozoea, sasa hivi tunafanya kazi kitaalamu zaidi,” amesema Kamanda Muslim.

 Amesema jeshi hilo linakusanya taarifa za ajali za barabarani kupitia mfumo wa kitaalamu ujulikanao kama RAIS (Road Accident Information System) ambao umesaidia kuripoti kwa wakati matukio yote yanayotokea barabarani na kusababisha vifo na majeruhi.

Amesema kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka 2017 hadi mwaka jana ajali za barabarani zimepungua kutoka 5,574 hadi 3,732 sawa na wastani wa asilimia 33, huku idadi ya vifo navyo vikipungua kutoka 2,581 hadi vifo 1,788 sawa na asilimia 31.

Kwa upande wa pikipiki amesema pia matukio yake yamepungua kwa asilimia 40 kutoka ajali 1,459 kwa mwaka 2017 hadi ajali 876 kwa mwaka jana, huku vifo vitokanavyo na ajali za pikipiki vikipungua kwa asilimia 50, kutoka vifo 728 hadi 366 kwa kipindi kama hicho.

Akizungumzia utofauti huo, Ofisa Mradi wa Usalama Barabarani kutoka Shirika la Afya Duniani, Mary Kessi, amekiri kuwepo kwa tofauti hizo kila mara na kusema wao hawakusanyi taarifa bali wanafanya uchambuzi kutokana na vyanzo mbalimbali na kwamba idadi wanayoipata ni makisio, si halisia.

Amevitaja vyanzo wanavyotumia katika uchambuzi wa taarifa hizo kuwa ni pamoja na taarifa kutoka katika hospitali idara ya uzazi na vifo pamoja na kuchukua taarifa zinazotolewa na Global Burden of  Disease inayoandaliwa na wadau mbalimbali ikiwemo Benki ya Dunia.

“Kanuni tunayotumia ni ngumu sana (technical) maana sisi tunaangalia idadi ya magari, idadi ya watu katika nchi husika pamoja na hali ya uchumi, na ndiyo maana unaona kwa nchi kama Tanzania kuna utofauti mkubwa ikilingalishwa na nchi zilizoendelea.

“Kwa ufupi ni kwamba taarifa ya polisi ni ‘actual’ kwa maana ya halisia, lakini taarifa zetu ni ‘estimate’ kwa maana ya makisio, na ndiyo maana hata sisi tunatumia hizo taarifa za polisi.

“Mfano hata kwenye ripoti yetu utaona tumeandika ripoti ya serikali ambayo ni ‘actual’, inasema hivi na yetu ambayo ni ‘estimate’ inasema hivi,” amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini nchini (SUMATRA), Gilliard Ngewe, amesema hawezi kuizungumzia ripoti hiyo na kusisitiza kuwa kwa sasa ajali zimepungua nchini.

Amesema kwa sasa wanaendelea na zoezi la kufunga mfumo wa kisatelaiti wa ufuatiliaji mwenendo wa magari barabarani unaojulikana kama ‘Vehicle Tracking System (VTS)’, ambao unaendelea kusaidia kupunguza ajali za barabarani.

Ngewe amesema kwa sasa madereva wa mabasi wameanza kutii na kuendesha kwa mwendo wa kisheria, ambapo zoezi hilo limechukua mwaka mzima kwa ajili ya kuelimisha umma juu ya faida ya mfumo huo ambao umeshaanza kuonyesha matokeo chanya.

Amesema tayari wamefikia lengo walilojiwekea la kuhakikisha kuwa hadi kufikia Juni mwaka jana, mabasi yote yanayotoka mkoa mmoja kwenda mkoa mwingine yawe yamefungwa mfumo huo na baada ya hapo wataendelea na zoezi hilo kwenye daladala.

Amesema watahakikisha kuwa hadi kufikia Juni mwaka huu mabasi yote yanayotoka makao makuu ya mkoa kwenda wilayani yawe yamefungwa mfumo huu.

Akizungumza baada ya kuzindua mfumo wa kisatelaiti wa kufuatilia mwendo wa mabasi hivi karibuni, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaac Kamwelwe, amesema asilimia 76.4 ya ajali zinazotokea nchini zinatokana na makosa ya kibinadamu.