SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Afya (WHO) linasema ingawa Afrika ina barabara na magari machache zaidi kuliko kanda nyingine, ndiyo yenye idadi kubwa kabisa ya vifo vya ajali za barabarani.
Ripoti hiyo ya hivi karibuni ya WHO inasema ajali hizo zinachochewa na uzembe, mwendo mkali, ulevi, miundombinu mibovu na magari mabovu.
Wataalamu wanasema maeneo mengine pia yanakabiliwa na changamoto kama hizo na nyingine kama za kutofunga mikanda ama kutovaa kofia ngumu.
Lakini kwa Afrika, ambako vifo 620 vya barabarani hutokea kila siku, hali huwa ni mbaya zaidi kutokana na barabara mbaya, magari makuukuu na upungufu wa huduma za dharura.
Ripoti hiyo ya WHO inasema Afrika imelitangulia eneo la kusini mashariki mwa Asia kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya vifo vya barabarani vya wastani wa watu 19.5 kati ya 100,000 kwa mwaka 2021.
Mwaka uliopita, Afrika – yenye asilimia 4 tu ya magari yote ulimwenguni – ilikabiliwa na asilimia 19 ya vifo vyote vya barabarani ulimwenguni.