Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
WATUMISHI wa Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ( MNMA) wametakiwa kuwa sehemu ya mabadiliko na kuungana na jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwenye mapambano dhidi ya vitendo vya Ukatili wa Kijinsia vinavyopelekea msongo wa mawazo na athari za Afya ya akili kwa jamii
Akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uelewa Watumishi wa MNMA kuhusu masuala ya Jinsia na Kifeminia yaliyofadhiliwa na Mfuko wa Ruzuku wa Women Fund Tanzania (WFT), Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaaluma Prof. Richard Kangalawe amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa mustakabali wa taifa.
Amesema Serikali ya Dkt. Samia imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha inapunguza vitendo vya ukatili nchini, hivyo kwa kupitia mafunzo haya Kila mshiiriki ana wajibu wa kuwa sehemu ya mabadiliko hayo ambayo yamekuwa yakiligharimu Taifa
Prof Kangalawe ameongeza kuwa mafunzo haya ni muhimu sana kwa Taasisi ya MNMA kwani yanatoa fursa ya kujifunza kwa pamoja masuala mbalimbali yanayoizunguka jamii ya Chuo
Amesema lengo la mafunzo ni kujengeana uelewa wa pamoja wa masuala ya Jinsia na Feminia ili kukabiliana na changamoto za Ukatili wa Kijinsia zinazopelekea matatizo ya Afya ya Akili.
” Binafsi nimefarijika kuona washiriki wa mafunzo haya wanatoka katika Idara tofauti za Taaluma na zisizo za Kitaaluma, ninawaomba muitumie nafasi hii adhimu kujifunza kuchukua yale mtakayojifunza na kuwashirikisha wengine ili yaweze kuwa chachu ya kutokomexa ukatili wa kijinsia katika jamii yetu,” amesema Prof.Kangalawe
Amesema masuala ya ukatili wa kijinsia yamekuwa na changamoto sana kwa Taifa na kwa kuwa Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere siyo kisiwa, hivyo madhara ya ukatili wa kijinsia yanatukumba sote kuanzia majumbani tunapoishi na katika utendaji kazi zetu za kila siku
Amesema ukatili wa kijinsia una madhara mengi kiuchumi, kiafya, kisaikolojia na kimwili madhara haya mara nyingi hupelekea msongo wa mawazo na athari za Afya ya Akili
“Hapa ninaonba kunukuua hotuba ya aliyekuwa Waziri wa Afya Ummy Mwalimu aliyoitoa wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia Novemba 30 mwaka jana,alisema Tanzania inatumia asilimia 3.5 ya Pato la Taifa kwa ajili ya kushughulikia masuala ya Ukatili wa Kijinsia ambapo fedha hizo zingeweza kutumika kwenye masuala ya Afya,Maji lakini pia kwenye masuala ya Elimu kwa watoto,” alisema Prof Kangalawe na kuongeza kwa kupitia kauli hii ni wazi kuwa masuala haya yanaligharinu Taifa
Kwa upande wake muwezeshaji katika mafunzo hayo kutoka Mfuko wa Ruzuku ( WFT) Mfemenia Mary Ndaro alisema mafunzo haya ni muhimu sana kwa Taasisi ya MNMA kwani yanatoa fursa ya kujifunza kwa pamoja masuala mbalimbali yanayoizunguka jamii ya Chuo
Amesema mafunzo hayo ni vema yakatumika kama mwanzo wa safari ya kukataa ukatili wa kijinsia unaosababisha msingo wa mawazo na kupelekea Afya ya Akili.
Naye Mtiva wa Kitivo Cha Uongozi na Sayansi za Utawala kutoka MNMA Dkt. Adili Zella akizungumza wakati akifunga mafunzo hayo aliwasihi washiriki kutambua kuwa changamoto ya Ukatili wa Kijinsia hajiwezi kishughulikiwa na mtu mmoja,shirika au Taasisi badala yake nguvu ya pamoja na inayohusisha taaluma mbalimbali, Afya za kisheria kijamii, kielimu na kisaikolojia inahitajika