Werrason Dima Makanda ni mmoja wa wanamuziki wa Kongo wenye washabiki wengi sana hapa nchini na Afrika kama si duniani kiujumla.
Lakini kwa muda mrefu mashabiki na wapenzi wake hao wamekuwa wakimfahamu Le Roi De La Forret Papaa na Exocee Mobali ya Mama Pastor Sylvie Mampata kijuujuu tu.
Safari hii mashabiki wake na wa muziki kijumla hususani wanafamilia wa Wenge wamepewa fursa maalum ya kumjua nguli huyu wa muziki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kupitia kitabu maalum ambacho kimeshachapishwa, kikielezea historia ya mwanamuziki huyo.
Kitabu hicho kinazungumzia maisha yake binafsi na katika harakati zake za kujiingiza kwenye muziki, hadi kufikia kuwa nyota mpaka sasa kumiliki bendi kubwa na yenye mafanikio makubwa.
Dondoo za yaliyomo kwenye kitabu hicho ni kwamba Werrason anaelezea kwa mfano Wenge Musica ilivyozaliwa. Katika hilo Werrason anasema mwanzoni kabisa walikuwa yeye Werrason, Aime Buanga, Jean Belix Luvutula, Didier Masela na Christian Zitu, ambapo Aime Buanga alichukuliwa kama mwanzilishi wa kundi kutokana na yeye kujitolea nyumba ya wazazi wake alimokuwa akiishi kutumika kama sehemu ya kufanyia mazoezi ya kundi lao hilo.
Pia Didier Masela naye kwa upande mwingine akichuliwa kama mwanzilishi pia kutokana na kwamba wazo la kuanzisha bendi lilitoka kwake.
Wakati fulani kwenye siku hizo hizo za mwanzo mwanzo za kundi lao, Aime Buanga alitaka kuachana na kundi hilo changa ili aendeleze kipaji chake kwenye sanaa za mapigano (martial arts) huku akimpa masharti rafiki yake Werrason kwamba kama unataka arudi kundini na yeye ajiunge naye kwenye sanaa za mapigano, sharti ambalo kwenye kitabu hiki Werra anadai alilitekeleza kwa kujumuika na swahiba wake kwenye martial arts.
Wakati ya Werrason na Aime Buanga yakiendelea hivyo, kwa upande mwingine Didier Masela alikuwa shule nje ya Kinshasa katika mji mdogo wa Mbanza Boma pamoja na Alain Makaba.
Baadaye huku nyuma JB Mpiana akafika kuja kujiunga na bendi ambapo Werrason anasema katika kitabu hicho akamueleza; “rafiki yangu nimesikia wewe ni mwimbaji mzuri sana kama hutajali naomba uniimbie wimbo kidogo nikusikie na mimi….” Baada ya kauli hiyo ya Werra ndipo JB inaelezwa akaimba wimbo uitwao ‘Abidjan’ wa Viva la Musica uliotungwa na Debaba.
Werrason mwenyewe na kila aliyekuwapo pale wakavutiwa sana naye kiasi cha kumpigia makofi kwa wingi, na watu wote baada ya hapo Werrason akampendekeza JB ajiunge na bendi na JB alikubali bila kusita.
Siku hiyo miongoni mwa waliomshuhudia JB akiimba pamoja na Werrason ni Didier Masela na Jean Belix. Na aliyemleta na kumtambulisha JB hapo kundini alikuwa ni Jean Belix Luvutula ambaye walikuwa wakiishi jirani na alikuwa akimuona JB aliyekuwa akiimba mtaani.
Baadaye Blaize Bula akaletwa na Makaba kujiunga na bendi kama mpiga ngoma (drums) kutokana na kwamba alikuwa mpiga drums wa bendi ya shule waliyokuwa wakisoma, lengo likiwa aje achukue nafasi ya binamu yake Werrason aliyekuwa akiitwa Ladins Montana, ambaye ndiye aliyekuwa mpiga drums.
Lakini Sele Bula akaonekana hana muonekano wa BCBG lakini Makaba kwa kujua kipaji cha Sele kwenye uimbaji pia akasisitiza aingizwe kundini. Hivyo wakawa wamempata Blaize (Sele) Bula kama mwimbaji.
Kwa upande mwingine JB ambaye alikuwa tayari kundini, alikutana na Tata Mobitch Adolphe Dominguez aliyekuwa mtoto wa tajiri mkubwa sana huko Kongo, lakini pia akiwa ni mnenguaji mzuri akicheza sana nyimbo za Defao.
JB na Adolphe baada ya kujuana kutokana na JB kuvutiwa na uvaaji wa Adolphe, wakatokea kuwa marafiki wakubwa huku Adolphe akimpigisha JB ‘pamba’ za ukweli kiasi cha kung’aa miongoni mwa wanabendi. Ndipo baadaye JB akamtambulisha Adolphe kwa Werrason na wengine kundini na wakaanza kumfundisha muziki Adolphe hapo hapo kundini, huku yeye akilipa fadhila kwa kuwafadhili upande wa mavazi kupitia utajiri wa babaake.
Kitabu kimeongelea mambo mengi ambayo hatutaweza kuyamaliza japo ni vyema nitoe dondoo za alichozungumzia Werrason kuhusu maisha yake binafsi.
Katika wasifu wa maisha yake binafsi Werra anasema alikutana na mkewe kipenzi Mama Pastor Silvie Mampata akiwa shule kupitia rafiki yake kipenzi wakati huo aitwaye Wasenga Kipuni. Sylvie alikuwa ni binti wa mfanyabiashara tajiri. Mama huyo alitumia utajiri wa baba yake kuisaidia sana bendi ya Wenge kupitia kwa Werrason.
Kuhusu mgawanyiko wa bendi hiyo, kitabu kinaeleza kwamba ni uamuzi wa JB kurekodi ‘Feux de L’amour’ kwa kuwashirikisha wanamuziki wengine kutoka nje ya Wenge kama alivyofanya Alain Makaba kwenye albamu yake iitwayo ‘Pile ou Face’; hapo ndipo mgogoro wa kiuongozi ulipoanza kuibuka.
Baada ya mafanikio ya Feux de L’amour, JB kwa kushirikiana na Simon Sipe ambaye ndiye aliyekuwa meneja wao akisimamia kila kitu mpaka uzalishaji wao, wakanogewa na kutaka kutoa albamu nyingine ya pili ya JB.
Hapo ndipo Werra alipokasirika na kuitangaza albamu yakeiliyojulikana kama Kibuisa mpipa, huku akiwa hana hata wimbo mmoja wakati huo akiitangaza ila tu alitaka kumuonesha JB kwamba hawezi kutoa albamu ya pili wakimtazama tu.
Baada ya hapo bendi ikagawanyika na Werra ili kushindana na JB akawa na mawazo ya kuanzisha bendi haraka haraka na kuanza kufanya maonesho, matokeo yake akachemsha sana mwanzoni kwenye maonesho yake ya awali yakawa ‘flop’ mpaka ndugu yake anayetoka naye kijiji kimoja, Marie Paul, akamuonea huruma na kuamua kumsaidia.
Marie alimpa bure mwanamuziki wake JDT na yeye mwenyewe akawapata watu kama Didier Lacoste, Adjan n.k. ndipo mambo yakaanza kwenda vizuri sasa na kutoa Force.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba:
0784 331200, 0767 331200 na 0713 331200.