Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma
Zikiwa zimesalia siku tano kufanyika kwa maandamano ya amani yanayoratibiwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kuishinikiza Serikali kuzingatia maoni na mapendekezo ya wadau wa Demokrasia nchini,baadhi ya Vyama vya upinzani mkoani hapa vimelaani maandamano haya kwa madai kuwa hayana viashiria vyovyote vya amani.
Aidha vyama hivyo vimetoa wito kwa Watanzania kupuuza maandamano hayo na kuendelea na kazi za ujenzi wa taifa kwa kuwa mchakato wa wanachokihitaji bado unaendelea bungeni na kwamba wanaamini maoni yao yatazingatiwa na wabunge .
Vyama hivyo ni pamoja na ACT-Wazalendo, CUF,ADC, NCCR-Mageuzi, AFP na Demokrasia Makini ambapo Wenyeviti wake kwa pamoja wameeleza kuwa maandamano hayo yanapotosha namna ya kudai haki na badala yake busara ya mazungumzo ingetumika.
Hayo yamejiri leo January 18,2024 Jijini hapa kwenye mkutano baina ya Vyama hivyo na vyombo vya habari ambapo Wenyeviti hao wameeleza kuwa mchakato halali wa majadiliano na fulsa iliyotolewa na Rais Samia Suruhu Hassan ya Maridhiano Kisiasa inapaswa kuzingatiwa na si vinginevyo.
Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Yohana Musa amesema kujenga umoja wa kitaifa kunatakiwa kuzingatia mazungumzo ya amani na si kuwaingiza watu barabarani kufanya maandamano katika nyakati hizi ambazo taifa linahitaji utulivu mkubwa.
Amesema wao kama wanasiasa hawaafiki wala kuunga mkono jambo hilo na kueleza kuwa watanzania waelewe kuwa maandamano hayo ni ya Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na Chama Chake.
Kwa upande mwingine Musa ameeleza kuwa Chama chake kimejiandaa kikamilifu kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi Mkuu na kwamba kamwe hawawezi kuususia uchaguzi huo.
“Hatuwezi kususa tukaacha shamba la mihogo nguruwe wavamie, tutashiriki uchaguzi na tutashinda, hivyo maandamano kwetu ni mwiko kwa sababu sisi kama ACT-WAZALENDO tunaamini katika mazungumzo ya amani na si maandamano, ” Amesisitiza
Naye Mwenyekiti wa Demokrasia Makini Baraka Malegesi kuna haja ya Serikali kuwa na utaratibu wa kuwashirikisha viongizi wa siasa katika maamuzi yake na kwamba hali hiyo itasaidia kupunguza manung’uniko na kudai haki kusiko halali .
“Nadhani Mwenyekiti wa CHADEMA angatumia busara na kuwaacha wananchi waendelee na shughuli nyingine,wengine wapo mashambani wakiendelea na kilimo, kwa wito huu anataka wananchi watoke kwenye shughuri za kilimo waje mijini kuandamana hii sio sahihi , ” Aamesema
Naye Mwenyekiti wa CUF Steven Chitema amesema, “Mbowe anaitisha maandamano katika jiji la kibiashara huku akitambua juhudi zilizofanywa na Rais Samia Suruhu Hassan kufungua fulsa za uwekezaji na biashara katika jiji hilo, lengo hapa sio maandamano ya Amani ila ni uharibifu na upotoshaji wa juhudi za Rais katika kuifungua nchi, “amesema na kuongea;
Mara kadhaa sisi wenye viti wa vyama vya upinzani halisi tumekuwa tukiwaambia Wananchi kuwa CHADEMA sio chama cha kuwapigia kura hasa katika chaguzi zinazokuja za serikali za mitaa na uchaguzi mkuu 2025 kwa kuwa wamekuwa wakiacha michakato halali na kikimbilia barabarani kutafuta huruma ya wananchi na kuacha hoja zilizopo mezani,”ameeleza
Kwa upande wake Kamishna wa Chama cha NCCR-MAGEUZI Meshack Masinga amesema Chama chao kinaungana na viongozi wa kitaifa kuendelea kulinda na kuheshimu misingi ya amani iliyoachwa na waasisi wa Taifa hili na kueleza kuwa maandamano yoyoye hayawezi kuwajenga watanzania.
Aidha amesema,”Sisi Wenyeviti wa Vyama Vya Upinzani tuliopo Makao Makuu ya nchi tunampongeza Rais Samia kwa uamuzi wake wa kupeleka Bungeni Marekebisho ya sheria ya uchaguzi ambapo sasa, kamati ya kudumu ya bunge ya katiba na sheria chini ya mwenyekiti wake Joseph Mhagama imetoa fulsa kwa wadau mbalimbali kutoa maoni yao wakiwao CHADEMA nafasi kwa wadau kutoa maoni yao kila mmoja kwa nafasi yake,”amesema na kuongea;
Kamati ya bunge ilitoa ushirikiano wa kutosha kwa wadau kiasi cha kutosha ilifikia baadhi ya wadau walipewa nafasi Zaidi ya mara moja kutoa maoni yao wakiwamo hawa wanaitisha maandamano, hii imekuwa ni tabia yao kuacha michakato halali na kukimbilia kwa wananchi kujilizaliza, Sisi tunasema hatuungi mkono maandamano hayo na tunalaani kwa nguvu kubwa ukiukaji huu wa maridhiano ya demokrasia, “amesema
Ikumbukwe kuwa haya yote yanajiri ikiwa ni hivi karibuni January 13,2024 Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe kutangaza vuguvugu la maandamano aliyoyaita ya amani ifikapo January 24,2024 kudai haki na kuishinikiza Serikali kizingatia maoni na mapendekezo ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi kuhusu Miswada mitatu.
Miswada hiyo ni pamoja na Sheria ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Muswada wa Sheria ya tume ya uchaguzi pamoja na Muswada wa Sheria ya marekebisho ya vyama vya Siasa.