SONY DSC

Mbali ya kifungu cha 32 cha Sheria ya Kudhibiti Ukimwi namba 28/2008 kupiga marufuku unyanyapaa, watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) wamesema tatizo hilo bado ni kubwa.
  Kutokana na hali hiyo, jamii ya wenye VVU imedai imekuwa ikilazimika kukubaliana na unyanyapaa unaofanywa na baadhi ya watu ili kulinda CD4 zisipunguwe mwilini.
  Walidai kuwa tangu janga hatari la Ukimwi lilipotua nchini na baadhi yao kuupata kwa njia mbalimbali, wamekuwa wakiitwa majina yenye lugha za unyanyapaa kama vile, 'ana ngoma'; 'anatembea na funguo za mochwari'; 'ana debe la utitiri'; 'anatembea na wali wetu' na mengine mengi yenye lugha ya unyanyapaa ambako wamekubaliana na hali hiyo ili kuepuka kufa haraka.
  Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Waviu Washauri kutoka wilaya sita za Mkoa wa Simiyu, waliotembelea Kituo cha Matunzo na Tiba (CTC) cha Hospitali ya Rufaa ya Bugando iliyopo jijini Mwanza.
  Waviu hao walikuwa wanashiriki warsha ya siku tatu iliyoandaliwa na Shirika la Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative (AGPAHI) la jijini Dar es Salaam linalojishughulisha na Ukimwi.
  Shija Mashimba, Mviu Mshauri wa hospitali hiyo, anadai kuwa tatizo la unyanyapaa kwa watu wenye VVU ni kubwa, na njia pekee ya kukomesha hali hiyo ni kukubaliana na matakwa ya jamii ili kutunza kinga za mwili (CD4).
  Mashimba alijibu swali la Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na VVU (NACOPHA), Vitalis Makayula, aliyetaka kujua sababu za mshauri huyo kutoa mafunzo kwa watu wanaoishi na Ukimwi kwa kutumia majina yenye lugha za unyanyapaa ilhali dunia inapiga vita unyanyapaa na kufikia sifuri kwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi.
  Akijibu swali hilo, Mashimba anasema analazimika kutumia lugha zenye unyanyapaa wakati akisaidia kazi zisizo za kitaalamu kwa wenye VVU, wanaofika katika hospitali hiyo ukiwamo ushauri kuwafanya wazoee hali hiyo kulinda kinga za mwili (CDF).
  “Napenda kutumia ngoma pale ninapotoa ushauri kwa wenzangu maana neno ngoma ndiyo jina la kwanza kuitwa watu wanaoishi na VVU, ndiyo lilitangulia, na si hilo tu, sisi wenye VVU tunaitwa majina mengi sana ya unyanyapaa.
  “Watu wanatuita tunatembea na wali wao wakimaanisha tukifa watakula wali, tunaitwa marehemu watarajiwa kana kwamba wao hawatakufa, tunaambiwa tunatembea na funguo za mochwari; hivi kweli ukinisachi utanikuta na funguo hizo? Kwa hiyo, majina yako mengi na njia pekee ya kuzoea hali hiyo ni wewe kukubaliana na hali halisi ili kulinda CD4, lakini ukijifanya kupaniki utakufa mapema,'' anasema Mashimba na kusababisha vicheko.
  Kuhusu kutumia namba badala ya majina, Mashimba ambaye ndiye mtu wa kwanza kujitangaza hadharani katika jiji la Mwanza kuwa mwathirika, anasema utaratibu huo uliwekwa kwa lengo la kupunguza unyanyapaa kwa wenye VVU mbali na tatizo hilo kuendelea kukua kila uchao.
  “Pamoja na mimi kujitangaza hadharani kwamba nina Ukimwi, kuna wenzetu bado si wawazi na ndiyo maana awali  kabla haujaanzishwa utaratibu wa kutumia namba badala ya majina, walikuwa wakiitwa watu majina wanakauka tu kuhofia eneo hilo yupo anayemfahamu, hivyo akirudi mtaani atavujisha siri kwamba fulani ana ngoma.
  “Na baada ya kubaini hilo ulianza kutumika utaratibu huu wa namba ambapo mtu anaweza kuitika na hata akiulizwa iwapo dawa ni zake atajihami kwa kusingizia amemfuatia dawa nduguye wakati si kweli," anasema.
  Kutokana na hali hiyo, Jane Shuma, Mratibu wa Mawasiliano na Huduma za Mkoa wa AGPAHI, anasema waliona ni muhimu kuandaa warsha hiyo ili kuwajengea uwezo Waviu Washauri waweze kuwaunganisha wateja kutoka kwenye jamii kwenda kwenye vituo vya afya.
  Kuwafuatilia wateja waliopotea na kuainisha changamoto zinazosababisha wasifike kwenye huduma na kutafuta njia sahihi za kutatua changamoto hizo.
 
Bosi Nacopha akemea

Hata hivyo, mwenyekiti huyo wa Baraza la Taifa anawataka watu wanaoishi na VVU kupiga vita hali hiyo kuliko kuiacha ikaendelea kana kwamba hakuna sheria ya kupinga unyanyapaa.
  Warsha hiyo ililenga kuwaunganisha wateja wanaohitaji huduma za ushauri na mafunzo zaidi kwa watoa huduma wa afya katika CTC na katika jamii, kuwafuatilia wateja waliopotea katika huduma za CTC na kuwaunganisha wanaopata huduma kutoka kliniki ya akinamama na watoto na kitengo cha matunzo na matibabu.
  Pia kuanzisha makundi ya Waviu walio kwenye dawa na wasiokuwa kwenye dawa, watoto na akinamama wanaoishi na watoto waliozaliwa na kuishi na VVU.
  Joyce Philimon, mkazi wa Somanda mkoani Simiyu, ni mmoja wa watu wanaoishi na VVU ambaye aliliambia gazeti hili kuwa aliambukizwa ugonjwa huo mwaka 1998.
  “Baada ya kupata majibu nilishtuka na kukata tamaa ya kuishi, kisha kuanza kutapanya mali nilizokuwa nimekusanya likiwamo duka kubwa nililokuwa nalimiliki. Niliuza bidhaa zote za duka na kutumia pesa zote nikisubiri kifo changu,” anasema.
  Anasema wakati anaambukizwa ugonjwa huo hakukuwa na dawa za kurefusha maisha, ambako aliendelea kuishi akizingatia masharti ya wahudumu wa afya, lakini hakufa kama alivyotarajia hadi mwaka 2005 ilipoanzishwa huduma ya dawa za kurefusha maisha kwa wenye VVU.
  Happiness Malamala, mkazi wa Bariadi mjini ambaye anaishi na VVU na Mviu Mshauri, alidai Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu inavyo vituo vitatu vinavyotoa huduma ya tiba na matunzo kwa wenye VVU, ambako hadi kufikia Julai 2014 idadi ya wateja waliopotea walikuwa 875.
  Anafafanua kuwa kati ya hao 769 walikwishaanzishiwa dawa za ARV huku 106 wakiwa hawajaanzishiwa dawa hizo.
Katika kipindi cha Julai 2014 hadi Machi 2015 idadi ya wateja waliofuatiliwa ni 319 ambapo kati yao 272 wanatumia dawa za ARV huku 47 wakiwa hawajaanza kutumia dawa hizo.
  “Watu 203 wenye VVU walipatikana na kurudi kwenye huduma ya dawa, 26 walishafariki dunia mbali na kutumia dawa, na 43 wamekwishahamia kwenye kliniki nyingine bila taarifa, mbali na kuwa wanatumia dawa,” anasema.
  Hata hivyo, alidai kuwa kwa sasa ni wateja 556 ambao wamepotea kati yao 497 wakiwa wanatumia dawa za ARV huku 59 wakiwa hawatumii dawa.
  Pamoja na hilo, alidai changamoto wanazokumbana nazo ni pamoja na wateja kujiandikisha zaidi ya mara moja, kujiandikisha kwa majina yasiyo yao, hali inayosababisha wasipatikane kwa urahisi wanapohitajika kwenye huduma.
  Malamala anadai kuwa mafanikio waliyoyapata ni pamoja na kuanzisha vikundi vinne vya watu wanaoishi na VVU Bariadi ambavyo ni Amani, Wavisa, Furaha, Old Maswa na cha Jamii ya watu wanaoishi na VVU Bariadi.
  Wakizungumzia mafanikio waliyoyapata kupitia Shirika la AGPAHI, baadhi ya Waviu Washauri walioshiriki warsha hiyo walidai ni pamoja na wateja kuweza kurudi baada ya kuwafuatilia kupitia simu na kupitia kwa viongozi wao wa mitaa.
  Hatua hiyo ilikuja baada ya kupata taarifa za wateja waliofariki na wale waliokataa huduma na kuamua kupunguza namba za wateja waliopotea (LTF).
 Wanadai mbinu zilizotumika ni pamoja na kuwafuatilia wateja kwa kuzingatia anuani zao, kuwapigia simu kupitia namba zao na za wasimamizi na za wakuu wa kaya na pia kutumia vikundi vya wateja wanaoishi na VVU na kutumia watoa huduma majumbani (HBC).
  Joyce Philimon, alidai kuwa wamefanikiwa kuanzisha vikundi viwili vya watoto wanaoishi na VVU (Ariel Club) vilivyopo katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi, kimoja kikiwa katika Kituo cha Afya Ngulyati na kingine katika Kituo cha Afya Muungano.
  Alifafanua kuwa kwa upande wa Ngulyati, kikundi hicho kinao watoto 23 — wavulana 10 na wasichana 13; kwa upande wa Muungano kuna watoto 25 — wavulana 12 na wasichana 12.
Aliyataja mafanikio waliyoyapata kuwa ni pamoja na kikundi cha zamani cha watoto wenye VVU kupokea wanachama wapya kutoka 36 hadi 56 waliopo sasa kati yao wasichana 34 na wavulana 22.
  Alidai kuwa vikundi vyote hivyo huwa vinakutana na kupewa elimu, kujadili mafanikio ya kila kikundi kwenye kliniki yao na pia wameweza kuanzisha kliniki pekee ya watoto kila siku ya Jumamosi kwa kila wiki kwenye hospitali ya mji wa Bariadi, ambapo baadhi ya watoto hao wamekwishapata fursa ya kuhudhuria kambi ya watoto wenzao iliyopo Arusha.
  Hata hivyo, watoto wote wa vikundi vya Ariel hupata huduma ya chakula mara mbili kila mwaka kwenye vituo vyao kwa ufadhili wa AGPAHI na kwamba wale waliopo Hospitali ya Bariadi hupatiwa huduma ya chakula kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.
  Kwa upande wa elimu juu ya kujikinga na maambukizi mapya, unyanyapaa, ufuasi mzuri wa dawa, uwazi, burudani na michezo hutolewa kwa watoto wote wanapokutana.
  Akizungumzia changamoto wanazokumbana nazo, Philimon alidai kuwa ni pamoja na watoto kutoka mbali na kituo, pamoja na kutokuwa na usafiri wa kuwafikisha kwenye huduma.
 
 

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Mageda Kihulya, anawataka Waviu Washauri kuendelea kuwa mstari wa mbele katika mapambano ya maambukizi mapya na kutoa elimu kwa kinamama wajawazito.
  Kihulya anasema Serikali kwa kushirikiana na Shirika la AGPAHI imeendelea kuhakikisha dawa za ARV, dawa za kuzuia magonjwa nyemelezi kwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi na vifaa muhimu vya vipimo vinapatikana kwa wakati.

AGPAHI yamwaga magari

Kutokana na hali hiyo, Shirika la AGPAHI limekabidhi msaada wa magari mawili mkoani Shinyanga kwenye Halmashauri za Msalala wilayani Kahama na Kishapu, na mawili kwenye Halmashauri za Itilima na Busega mkoani Simiyu, yenye thamani ya Sh. milioni 356 kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali za mapambano dhidi ya Ukimwi kwenye halmashauri hizo.
  Akikabidhi msaada wa magari hayo, kwa nyakati tofauti mbele ya viongozi wa halmashauri hiyo pamoja na wabunge, Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa AGPAHI, Laurean Lugambwa Bwanakunu, alisema magari hayo mapya aina ya Toyota Land Cuiser (4X4) yametolewa kwa ufadhili wa watu wa Marekani kupitia shirika la kituo cha kuzuia na kudhibiti VVU la hapa nchini, huku kila moja likigharimu Sh million 89 bila kodi.
  Bwanakunu anasema kuwa kazi za magari hayo ni kurahisisha rufaa za wagonjwa kutoka kituo kimoja hadi kingine, kufanya usimamizi shirikishi vituoni, kusambaza dawa na vitendea kazi kwenye vituo vya kutolea huduma pamoja na kurahisisha usafirishaji na sampuli za CD4.