Donald Trump ameapishwa kuwa Rais wa 45 wa Marekani. Huyu ni Rais wa taifa lenye nguvu kubwa za kiuchumi na kijeshi kuliko taifa lolote katika sayari hii.
Ushindi wa Trump haukutarajiwa na wengi. Maneno yake kabla na wakati wa kampeni yalitosha kumfanya achukiwe na wengi, akionekana mbaguzi, mbabe na kiongozi asiye na huruma.
Januari 20 dunia ilishuhudia Trump akila kiapo cha kulitumikia taifa lake, na punde akatoa hotuba yake ya kwanza kama kiongozi mkuu wa taifa la Marekani.
Kama ilivyotarajiwa, hakumung’unya maneno. Akatamka wazi kuwa kipaumbele chake ni Marekani na Wamarekani.
Maneno yake yalikuwa machache, lakini yaliyobeba ujumbe mzito, si kwa Wamarekani pekee, bali kwa walimwengu wote.
Hotuba ya Rais Trump ilikuwa ujumbe tosha kabisa kwa mataifa ya Dunia ya Tatu, hasa Afrika ambako utegemezi umekuwa sehemu ya imani ya Waafrika. Afrika hatuhitaji misaada bali tunachohitaji ni uwanja wa haki wa kibiashara na kukomesha dhuluma za mataifa makubwa.
Hatuna budi kutambua kuwa Rais Trump yupo kwa ajili ya Wamarekani, na si wategemezi kama Afrika ambao licha ya kuwa na utajiri mwingi wa rasilimali za kila aina, ndilo bara lenye makabwela wengi kuliko mabara yote.
Hotuba yake yake inapaswa kutuamsha Waafrika, hasa Watanzania ambao kwa wingi na thamani ya rasilimali tulizonazo, hatuna sababu ya kuwa ombaomba.
Ndiyo maana tunaunga mkono mwito wa Rais John Magufuli kwa Watanzania, kupenda kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kujiletea maendeleo.
Heshima ya binadamu haitokani na kuwa ombaomba. Heshima inaletwa na hali ya maisha anayokuwa nayo binadamu kutokana na uhodari wake katika kufanya kazi.
Watanzania tuna ardhi nzuri inayofaa kwa kilimo cha mazao mengi, tuna madini mengi yakiwamo mengine yasiyopatikana kwingineko duniani, tuna maziwa makubwa, tuna bahari, tuna mito, tuna hifadhi na mapori ya wanyamapori, tuna mifugo mingi, tuna rasilimali watu ya kutosha; tupo mahali pazuri kijiografia na kadhalika.
Ili rasilimali zote hizi ziwe na tija, hatuna budi kila mmoja wetu kuamua kufanya kazi kwa nguvu na uwezo wake wote.
Rais Trump alichofanya ni kama kutuambia Waafrika kuwa hatuna mjomba, kwa hiyo ni wajibu wetu kusaka maendeleo kwa nguvu na kwa weledi.
Miaka 55 baada ya Uhuru ni aibu kwetu na kwa Afrika kuendelea kudeka kwa mataifa yaliyoendelea kwa nia ya kuomba misaada. Ni aibu kuona hadi leo mjadala wetu unakuwa wa baa la njaa.
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alisema “Inawezekana, Timiza Wajibu Wako”. Naam, hotuba ya Rais Trump iwe mwanzo wa kuturejesha kwenye misingi ya kuamini kwenye sera ya kujitegemea.