Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dodoma

MENEJA wa Kanda ya Kati kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Gerald Mollel amesema wengi waliojitokeza katika banda lao la maonesho ya kitaifa ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) wametaka kufahamu huduma zao ikiwemo ya uchunguzi wa vinasaba (DNA) pamoja na kemikali.

Akizungumza na waandishi wa habari katika banda lao lililopo katika maonesho hayo yanayoendelea katika Viwanja vya Nanenane-Nzuguni jijini Dodoma amesema wananchi hao wanataka kujua huduma ya uchunguzi wa vinasaba wanaanzia wapi ili kuipata pamoja na gharama zake.

“Wengi wanaotembelea hapa maswali yao makuu yanahusu vinasaba na kemikali. Watu wanapenda kujua uchunguzi wa vinasaba ukoje, gharama zake pamoja na muda. Na kama nilivyosema Mamlaka inasimamia masuala ya kemikali za viwandani na majumbani na kutoa elimu kwa wadau mbalimbali kujua ni kemikali gani inaingizwa nchini na kwaajili ya kitu gani.

“Kwahiyo nitoe wito kwa Wananchi na wadau mbalimbali wafike kwenye banda letu ili kuweza kupata elimu juu majukumu yetu,” ameongeza.

Amebainisha kuwa Mamlaka hiyo inasimamia sheria tatu ambazo ni sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali namba 8 ya Mwaka 2016, Sheria ya Udhibiti wa kemikali za viwandani na majumbani namba 3 ya Mwaka 2003 na Sheria ya Usimamizi wa Udhibiti wa vinasaba vya binadamu namba 8 ya Mwaka 2009.

“Kwa Wakulima na Wafugaji, Mamlaka tunafanya uchunguzi wa aina mbalimbali inawezekana maziwa au mazao yao kama mahindi na mazao mengine. Kwa mfano mahindi tunangalia sumu ile na kuona kama mazao yanafaa kwa matumizi, asali pia tunapima na kutoa hati ya uchunguzi kama inasafirishwa nje ya Nchi.

“Pia kuna usajili wa kemikali mbalimbali, usajili wa wadau wanaoingiza nchini kemikali za majumbani na viwandani, lengo ni kuhakikisha bidhaa zinazoingia nchini zinakuwa bora na ni kemikali sahihi kwa matumizi ya Nchi na pia tunakuwa na database ya kuweka hizo kemikali kuhakikisha kemikali zinazoingia nchini ni zile ambazo zimesajiliwa kwa mujibu wa Sheria,” amesema.

Naye, Kaimu Mkurugenzi, Uchunguzi wa Bidhaa na Mazingira katika mamlaka hiyo, Shimu Peter amesema kuwa majukumu ya GCLA yanahusisha uchunguzi wa sampuli za jinai, sampuli za vyakula, Mazingira, dawa za asili na za kisasa na sampuli zinazohusiana na vinasaba vya binadamu (DNA).

“Teknolojia ya DNA au Sayansi ya binadamu ni pana na watu wengi wanajua kuwa sayansi hiyo inahusika na kufahamu urithi tu wa watoto kwa wazazi wao lakini kazi zingine ni kwamba unapofahamu uhalisia wa mtoto kwa wazazi hii inakusaidia kwa matumizi mbalimbali ikiwemo mirathi, pia inasaidia katika taasisi zingine ambazo zinaweza zikawa zinahitaji.

“Inatumika pia katika kupima vinasaba vya binadamu ili kuweza kufahamu kama kuna changamoto yoyote ya kiafya kwa mfano watu ambao wanahitaji kupandikizwa figo lazima watumie Sayansi hii. Watu ambao wana changamoto ya jinsia mbili ili kuweza kupata tiba sahihi ni lazima apimwe vinasaba vya binadamu pamoja na watu ambao sio waaminifu mfano mbakaji ili sheria iweze kuchukua mkondo wake ni lazima kupima ili kujiridhisha na mtuhumiwa halisi ambaye amefanya tukio lile,” amefafanua.

Please follow and like us:
Pin Share