Kampuni ya TanzaniteOne Ltd inayochimba madini ya tanzanite katika eneo la Mererani mkoani Manyara, hatimaye kuanzia wiki hii italazimika kuachia asilimia 50 ya hisa zake zimilikiwe na wazalendo, imethibitishwa.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, anatarajiwa kwenda Mererani wakati wowote kuanzia kesho kutangaza rasmi umiliki wa Watanzania wa asilimia 50 katika mgodi huo. Mkutano mkubwa umeandaliwa kwa ajili ya tukio hilo la historia katika uwekezaji kwenye madini ya vito hapa nchini.

Kampuni hiyo kutoka Afrika Kusini, inalazimika kufanya hivyo ili kuendana na Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 inayotaka madini ya vito yasichimbwe kwa asilimia 100 na wageni.

TanzaniteOne ilitakiwa iwe imesitisha shughuli zake tangu Julai, mwaka huu; mwezi ambao leseni yake ilikuwa inakwisha, lakini kukawapo mvutano wa wamiliki wake kutaka kuendelea kuhodhi utajiri huo.


“Ninachoweza kukuhakikishia ni kwamba serikali imeshaweka taratibu za kuhakikisha asilimia 50 ya hisa za TanzaniteOne inaingia kwa Watanzania. Wiki ijayo (wiki hii) nitakwenda Mererani kumaliza tatizo hilo ambalo limedumu kwa muda mrefu. Mimi kazi yangu ni uchumi na maendeleo.


“Nitakutana na wananchi, vyama vyote vya siasa, mashirika yasiyo ya serikali, viongozi wa madhehebu yote, lengo ni kuhakikisha kelele za muda mrefu kuhusu Mererani tunazimaliza na watu wote wafurahi,” amesema Profesa Muhongo alipozungumza na JAMHURI kwa simu.


Ingawa Muhongo hakutaka kuingia kwenye undani wa utekelezaji wa sheria hiyo ya mwaka 2010, kuna habari kwamba, kwa uamuzi wa kuanzia, hisa 50 zitamilikiwa na wafanyakazi wazalendo wa TanzaniteOne wanaokaribia 700, Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro pamoja na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).


Chanzo cha habari kimesema wananchi wengine wanaweza kununua hisa kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).


Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa Wizara ya Nishati na Madini ilikataa ombi la Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TanzaniteOne, Balozi Ami Mpungwe, la kutaka kumiliki asilimia 50 ya hisa kupitia kampuni aliyoianzisha na familia yake.


Msimamo wa Wizara ulikuwa kwamba kitendo cha Balozi Mpungwe kumiliki hisa hizo na familia yake kisingeleta tija kutokana na maudhui ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 ya kutaka Watanzania wengi washiriki kumiliki utajiri huo.


Juhudi za kutaka kuendelea kumiliki mgodi

Mwaka jana, TanzaniteOne iliandika barua kwa Wizara ya Nishati na Madini ikiomba iendelee kuchimba madini hayo. Hata hivyo, haikujibiwa. Habari za uhakika zilizopatikana baadaye zilisema kuwa mipango ilikuwa ikisukwa kwa kuwahusisha baadhi ya viongozi waandamizi serikalini pamoja na familia zao, ikiwa ni pamoja na kuwapa hisa ili kampuni hiyo iendelee kuchimba tanzanite.


TanzaniteOne imekuwa ikipata misukosuko mingi kutoka kwa wachimbaji wazalendo, lakini mara zote imeshinda changamoto zote.


Habari zaidi zinasema serikali imeipa TanzaniteOne masharti mapya endapo inataka kuendelea kuchimba madini hayo. Masharti hayo ni kuhakikisha kuwa asilimia 50 ya hisa inamilikiwa na Watanzania.


TanzaniteOne wamekuwa wakisita kuukubali uamuzi huo kutokana na ukweli kwamba kwa miaka yote ni wao pekee waliofaidi utajiri huo na kujinasibu duniani kote kwamba ndiyo wachimbaji na wauza tanzanite halali.


Mwenyekiti wa Chama cha Wauzaji Madini ya Vito Tanzania (TAMIDA), Sammy Mollel, anasema, “Tumesubiri kwa muda mrefu sana, sasa muda umefika wa serikali kutimiza ahadi yake ili eneo hilo ligawanywe kwa wachimbaji wadogo nao wajikomboe kiuchumi, baada ya kukandamizwa kwa muda mrefu na mfumo wa uchimbaji usio na uwiano sawa.”


Mollel ameongeza, “Hawa jamaa hawataki kuondoka, serikali haijawaongezea muda, lakini wanaendelea kuchimba na kusafirisha.


Hii ni kinyume cha sheria…ni uhuni. Hatuamini kama wameiweka serikali mfukoni, hawawezi hawa.


Kwa sasa tuna uongozi imara sana katika Wizara ya Nishati na Madini, matarajio yetu ni kuona hawa wanaondoka.


“Rais alitoa ahadi ya wazawa kumiliki tanzanite hii mbele ya hadhara na pia muda umefika sasa wa serikali kuwawezesha wazawa badala kuwakumbatia wageni ambao wamekuwa wanamaliza rasilimali zetu.”


Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, Rais Jakaya Kikwete aliahidi kuwamegea wachimbaji wadogo eneo la mgodi huo baada ya TanzaniteOne Ltd kumaliza mkataba wake. Alitoa ahadi hiyo akiwa Kijiji cha Lengast wilayani Simanjiro.


TanzaniteOne imekuwa kwenye mivutano mikali na wachimbaji wadogo kutokana na mitobozano ya mara kwa mara.


Walinzi wake wamekuwa wakiwajeruhi kwa risasi za moto wachimbaji wadogo.

Wachimbaji wadogo wamekuwa wakilalamika kwamba wanaonewa na kampuni hiyo, na wakati mwingine wenzao wameuawa na hata kung’atwa na mbwa wa kampuni hiyo.


Wachimbaji wadogo wamekuwa wakiendesha shughuli zao katika vitalu A, B, D na eneo la Karro ambalo hata hivyo, si maarufu kwa uzalishaji wa tanzanite.


Serikali iliwaahidi wachimbaji wadogo tangu mwaka 1995 kwa nyakati tofauti kuwa watapewa eneo la kitalu C.


Madini ya tanzanite yaligunduliwa mwaka 1968 na mkazi wa Makanya wilayani Same, Jumanne Ngoma; na serikali ilimkabidhi cheti cha kumtambua kwa ugunduzi huo. Hata hivyo, kuna madai mengine kwamba mgunduzi ni Ali Juuyawatu.


Miaka zaidi ya 40 sasa tangu madini hayo yagunduliwe, Mererani imetambuliwa kuwa ndipo mahali pekee duniani yanakopatikana madini hayo.


Pamoja na kuzalishwa Tanzania, Kenya na Afrika Kusini ndizo nchi zinazotambulika kuwa wauzaji wakuu wa madini hayo.


Mji wa Jaipur nchini India ndiko madini hayo yanakochongwa. Watu milioni moja wanafaidika na ajira hiyo ya tanzanite katika mji huo.


Tanzania ilipotangaza kupiga marufuku usafirishaji tanzanite ghafi nje ya nchi, India ilituma ujumbe mzito kuja kuibembeleza Serikali ya Tanzania kuacha mpango huo. Lengo la India lilikuwa kulinda ajira za wananchi wake ambao wangeathiriwa na msimamo wa Tanzania.