Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko Zanzibar, Amina Ally amewashauri wafanyabiashara wa Zanzibar kuwa wabunifu katika biashara zao ili kuongeza thamani ya biashara zao jambo litakalosaidia kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Zanzibar kwa ujumla.

Waziri Amina aliyasema hayo alipokuwa akizindua hafla ya Klabu ya Biashara ya NMB ambapo pamoja na kutoa ushauri huo kwa wafanyabiashara pia aliipongeza benki ya NMB kwa kuandaa hafla hiyo ambayo itasaidia kuwajenga wafanyabiashara.

“Kwanza kabisa naomba niwapongeze NMB kwa kuandaa hafla hii adhimu. Lakini pia nyie wafanyabiashara kwa kuona umuhimu wa kuhudhuria hafla hii kwani mmeacha shughuli zenu za kuwaingizia mapato na kuja kuungana na NMB ili msikie wamewaletea nini katika kukuza biashara zenu,

“Ninaimani hamtorudi nyumbani kama mlivyokuja kutokana na ukweli kwamba mtapata fursa ya kupata mafunzo mbali mbali ya jinsi ya kuendeleza biashara zenu,” alisema Waziri Amina.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo na Kati wa benki ya NMB, Donatus Richard alisema klabu ya wafanyabiashara ya NMB imekua na utaratibu wa kukusanya wafanyabiashara wote ambao wanapata mikopo katika benki hiyo na kuwapa mafunzo na kuwajulisha huduma mbalimbali za benki ambazo zinamfaa kila mjasiriamali kulingana na biashara yake.

“Sisi kama NMB kwa mwaka huu 2018 tumejipanga vizuri kabisa kuwahudumia wateja wetu, na tumekuja na bidhaa tofauti tofauti ili kukidhi mahitaji ya wateja wetu. Tunao wateja ambao ndo kwanza wanaanza biashara lakini wapo wale ambao tayari wanafaidika na mikopo mikubwa kabisa kutoka NMB,

“Tunachotaka kuwaambia ni kwamba NMB ipo tayari kumuinua mjasiliamali mdogo kabisa aje kua mjasiliamali mkubwa kabisa. Ni matarajio yetu kwamba mkopo wowote wa mteja wa NMB usichukue zaidi ya siku nne na mteja awe ameshapata mkopo wake hii itasaidia wateja wengi kuishi katika ndoto zake za kukua kibiashara,” alisema Richard.