Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Waziri wa afya nchini Dkt: Jenista Mhagama anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa ustawi kwa watoto wenye changamoto ya ugonjwa wa usonji.
Mradi huo ambao umeandaliwa na taasisi ya kijamii ya Lukiza Autism Foundation umelenga kuifikia jamii ya watoto wenye usonji ambapo kupitia mabalozi wa taasisi hiyo itazunguka katika shule mbalimbali za awali na kuendesha zoezi la utoaji elimu kwa walimu juu ya dalili mbalimbali za ugonjwa huo ili kusaidia kuwabaini watoto wenye changamoto hiyo mapema na kupatiwa mahitaji stahiki.
Akizungumza Mkurugenzi mtendaji wa asasi ya kijamii ya Lukiza Autism Foundation, Bi: Hilda Nkabe ametoa rai kwa watanzania na wadau mbalimbali kuungana kwa pamoja katika hafla hiyo kuchangia mradi huo ambao utasaidia kuwafikia watoto wenye changamoto ya usonji kwani hata wao pia wanahitajika kupewa haki sawa kama watoto wengine.
Harambee hiyo inafanyika mwaka huu ukiwa ni msimu wake wa tatu huku ikitarajia kuwatambua kwa tuzo za heshima wadau mbalimbali ambao wamekuwa na mchango mkubwa wenye tija katika kupigania haki za msingi kwa jamii ya watoto wenye usonji nchini.
Aidha mbali na wadau hao hafla hiyo pia itaenda sambamba na uzinduzi rasmi wa mbio za hisani ambazo zimekuwa zikifanyika kila mwaka chini ya uratibu wa asasi ya Lukiza foundation zikiwa na lengo la kuwasaidia waathirika wenye changamoto ya ugonjwa huo.
Shughuli hiyo inatarajiwa kufanyika wikiendi hii ya Disemba 7 mwaka huu katika hoteli ya kitalii ya Serena jijini Dar es salaam.