Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Waziri wa mifugo na uvuvi Abdallah Ulega ameongoza ufunguzi wa msimu wa sita wa shindano la Ladies First.
Ufunguzi wa shindano hilo umefanyika asubuhi ya leo katika uwanja wa Benjamin mkapa, Dar es salaam.
Waziri Ulega ameongoza shughuli hiyo ya ufunguzi wakati akimuwakilisha waziri wa Utamaduni, sanaa na michezo Dkt: Damas Ndumbaro aliyetarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Waziri Ulega amepongeza wazo la mashindano hayo huku akiyataja kama fursa muhimu kwa wanamichezo wakike nchini kwani watapata fursa ya kushindana na kuonyesha vipaji vyao ambavyo amesisitiza kama vikilelewa vizuri na kuendelezwa nchi itapata wanariadha bora watakaoiwakilisha nchi katika mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
“Mashindano haya ni fursa muhimu sana kwa nchi yetu ambapo wanamichezo wetu wa kike kutoka mikoa yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watapata fursa ya kushindana na kuonyesha vipaji vyao ambavyo vikilelewa na kuendelezwa nchi yetu itapata wanariadha bora watakaoikilisha nchi katika mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.”
“Na hapa nimeelezwa kuwa mashindano hayo yanalenga vijana wenye umri wa nchini ya miaka 20, hivyo ni wazi kuwa mashindano yamelenga kuibua na kuendeleza vipaji.Sote tunafahamu kuwa ushiriki wa wanawake katika michezo katika nchi yetu ni mdogo sana ukilinganisha na ushiriki wa wanaume. Hili linachangiwa na sababu kadhaa ikiwemo majukumu aliyonayo mwanamke katika familia, kutokuwepo elimu ya kutosha juu faida ya mwanamke kushiriki katika michezo pamoja na kukosekana kwa fursa za michezo kwa watoto wa kike.
Ndugu Wanamichezo,Ni jukumu letu sote la kuhakikisha tunapinga mila na desturi ambazo zinadumaza ushiriki wa wanawake kwenye michezo pamoja na kuendelea kuielimisha jamii umuhimu wa wanawake kushiriki kwenye michezo. ” alisema.
Aidha waziri Ulega ametoa shukran kwa serikali ya Japan kwa kuendelea kusaidia maendeleo ya michezo nchini kupitia mashirika mbalimbali kutoka nchini Japan.
“Napenda pia kuishukuru sana Serikali ya Japan kwa kuendelea kusaidia maendeleo ya michezo nchini. Nimeelezwa kuwa kwa kipindi kirefu Taifa letu limenufaika na wataalamu wetu kwenda Japan katika Mpango wa kubadilishana wataalam katika masuala ya michezo Wataalamu wa Japani pia wamesaidia sana kuendeleza michezo ya baseball na mchezo wa riadha hapa nchini.” Amesema.
Kwa upande mwingine pia balozi wa Japan nchini Tanzania, Yasushi Misawa nae ameiasa jamii ya kitanzania kuwa uwezeshwaji wa wanawake hauishii kwa wanawake pekee bali hata wanaume pia wanaweza kujifunza na kukuza maarifa yao na kuamini kuwa usawa wa kujinsia unamaanisha kuwa wanaume na wanawake wanaweza kutumia vizuri fursa wanazozipata.
Shindano hilo la Ladies First linafanyika jijini Dar es salaam, huku likipewa nguvu kwa kiasi kikubwa na shirika la maendeleo la Japan (JICA).
Shindano hilo linatarajiwa kuhitimika hapo kesho Novemba 24 katika uwanja Benjamin Mkapa.