Na Rahma Sufiani, SJMC Dodoma
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry William Silaa amewasili kwa mara ya kwanza ofisi za Wizara hiyo na kusisitiza ushirikiano pamoja na kuzingatia muda wakati wa utekelezaji majukumu ya wizara hiyo.
Silaa aliwasili ofisi za Wizara hiyo zilizopo eneo la Mtumba katika Mji wa Serikali jijini Dodoma tarehe 4 Septemba 2023 na kupokelewa na watumishi wa wizara hiyo wakiongozwa na Naibu Waziri Geofrey Pinda na Katibu Mkuu Mhandisi Antony Sanga.
“Napenda kuwashukuru sana namna mlivyonipokea katika siku yangu ya kwanza ninajisikia furaha kujumuika nanyi hivyo niwaombe tufanye kazi kwa ushirikiano ili kumsaidia Mh: Rais Dkt Samia Suluhu Hassan” alisema Silaa
Aidha, Waziri Mhe. Silaa alikutana na Menejimenti ya utumishi ya Wizara ya Ardhi na kufanya kikao kifupi ambapo aliweka wazi vipaumbele vyake vikuu viwili na kuvitaja kuwa ni Ushirikiano na Muda.
“Mimi nina taratibu zangu za utendaji, kwanza kabisa ninaomba ushirikiano zaidi kazini kwani mimi nipo hapa kumsaidia Mh. Rais hivyo naomba muwajibike ili Rais akipita huko kwa wananchi wawe wanampigia makofi kumpongeza kutokana na utendaji mzuri tutaounesha”. Alisema Waziri Silaa
“Nimefika mapema ofisini na nimeona baadhi wa watendaji wanakimbizana kwani wamekuja kwa kuchelewa ofisini sasa naomba tuongeze kasi zaidi ya kufika kazini, lakini pia naomba muwe huru kunishauri kwa lolote ili kuhakikisha tunafanya kazi kwa umoja na Ushirikiano” Alisema
Kwa mujibu wa Mhe. Silaa utendaji kazi ndani ya Wzara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi unawezekana kutokana na ushirikiano, hivyo aliomba ushirikiano ili kumsaidia Mh Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”.
Agosti 30, 2023, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassani alifanya mabadiliko madogo katika safu ya baraza la mawaziri ambapo alimteua Mhe Jerry William Silaa Mbunge wa jimbo la Ukonga kuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi akichukua nafasi ya Mhe, Dkt Angeline Mabula mbunge wa jimbo la Ilemela.