JERRY SILAA ANAZUNGUMZA
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry William Silaa (Mb.) anafungua mkutano kwa kusema:
Napenda niwahakikishie kuwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatambua umuhimu wa vyombo vya habari Tanzania, na ameendelea kuuenzi. Mtakumbuka hili aliliweka wazi katika kipindi cha wiki mbili tu baada ya kuingia madarakani ambapo tarehe 6 Aprili, 2021, alitoa maelekezo ya kuvifungulia vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungiwa na pia kuvirejeshea leseni vyombo vya habari ambavyo vilikuwa vimemaliza adhabu zao ili viendelee na majukumu yake. Mhe. Rais ameendelea kutoa maelekezo na tarehe 26 july, 2024, wakati akiniapisha Ikulu alinielekeza nisimamie uhuru wa habari.
Ndugu washiriki;
Serikali imeendelea kuboresha Sekta ya Habari, kama mnavyofahamu, Sekta hii, ni mtambuka inayosimamiwa na Sera, Sheria na Kanuni pamoja na miongozo mbalimbali, na katika uandaaji wa hizi Sheria, marekebisho yake na kanuni zote mmeshiriki kikamilifu kwa pamoja ambapo kupitia marekebisho hayo na utungwaji wa kanuni hizo kunawezesha wanahabari kufurahia haki yao ya uhuru wa maoni, haki ya kupata habari na uhuru katika kazi zao za uhariri bila kuwa na woga wa adhabu za kijinai.
Pamoja na mambo mengine, marekebisho yamewaondolea wanahabari makosa yanayohusu kashfa za kijinai, makosa ambayo kwa kawaida yanaangukia katika utaratibu wa mashauri ya madai. Aidha, marekebisho yamewaondolea adhabu wamiliki wa mitambo ya uchapishaji ambao katika hali ya kawaida hawana uwezo wa kudhibiti maudhui yanayochapishwa katika mitambo yao.
Ndugu washiriki;
Mtakumbuka marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari Sura ya 229 ya mwaka 2023 yameanzisha Bodi ya Ithibati. Kwa kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais tarehe
18 Septemba, 2024, niliteua wajumbe wa bodi husika ikiwa ndio bodi yangu ya kwanza kuteua. Nimemteua mwanahabari nguli Tido Mhando, kuwa Mwenyekiti wa bodi hii ambaye anauzoefu mkubwa wa sekta ndani na nje ya nchi nikiamini atatusaidia kuchagiza sekta hii kwa mujibu wa sheria. Uzinduzi rasmi wa bodi hii muhimu utafanyika mapema mwezi Disemba, 2024 na hii itatufungulia njia ya safari ya kuanzisha Baraza Huru la Habari na pia Mfuko wa Mafunzo kwa Wanahabari na tathimini ya hali ya uchumi kwa vyombo vya habari. Pia, nipende kuwafahamisha kuwa Wizara imeendelea kuratibu uanzishwaji wa mchakato wa marekebisho ya Sera ya Habari Haya yote ni baadhi ya masuala ya msingi yanayokwenda kuboresha Sekta ya Habari nchini. Hivyo, niwaalike kujiandaa kutoa maoni kwani sera hii ni yetu sote!
Ndugu washiriki;
Moja ya majukumu ya vyombo vya habari na wanahabari ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata habari sahihi na kwa wakati lakini pia wanahabari na vyombo vya habari wanakuwa huru kwa mujibu wa Sheria. Kwa msingi huo nimeona ni vyema tukakutana leo pamoja na kujadili masuala mbalimbali muhimu kuelekea katika uchaguzi Mkuu wa Serikali za mitaa. Lengo hasa nikujadiliana na kukumbushana masuala ya kuzingatia wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi lakini kujadili kama kuna uwepo wa Changamoto na Wizara iziwasilishekwenye mamlaka husika kwa ajili ya utatuzi.
Ndugu washiriki;
Kwa muktadha wa nilichotangulia kukieleza, ndiyo kimejenga msingi wa kuhusisha wizara na wadau wengine kuwepo hapa kama vile Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (msimamizi wa Sekta) na Wizara ya Habari. Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ili tuzungumze kwa pamoja.
Ndugu washiriki;
Historia inatukumbusha kwamba tasnia ya habari imekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi yetu kabla na baada ya uhuru ambapo vyombo vya habari vilitumika katika kuhamasisha kushiriki harakati za kudai uhuru na hata baada ya uhuru, Muasisi wa Taifa hili Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alitumia vyombo vya habari katika kuwaunganisha Watanzania na kuleta umoja wa kitaifa ambapo mpaka leo hii Tanzania imekuwa mfano duniani kwa namna ambavyo tumeungana, kushikamana na kuendelea kuimarisha umoja wa kitaifa. Yote haya yamewezekana kutokana na mchango wa vyombo vya habari. Niwathibitishie, niko karibu nanyi, sisi ni familia moja na milango yangu iko wazi karibuni tuijenge sekta yetu.
Ndugu washiriki;
Nimeelezwa kuwa katika mkutano huu, mada mablimbali zitawasilishwa. Mada hizo ni pamoja na Mwongozo wa Uandishi wa Habari za Uchaguzi, Wajibu wa Waandishi wa Habari na Jeshi la Polisi katika kulinda usalama wa waandishi wa habari na wananchi wakati wa uchaguzi, Uzoefu wa waandishi wa habari katika kuripoti matukio ya uchaguzi yaliyopita (Mafanikio na Changamoto) na Matarajio ya Serikali kwa sekta ya habari katika kuripoti matukio ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2025. Kwa umuhimu wake na mimi kama waziri mwenye dhamana baada ya ufunguzi, nitashiriki mkutano huu mwanzo mpaka mwisho.
Ndugu washiriki;
Naomba niwapongeze waandaaji wa mkutano huu kwa kuandaa mada hizi ambazo zimekuja katika wakati muafaka ambapo tunakwenda kuanza kampeni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa lakini pia mwakani tutakuwa na uchaguzi mkuu ambapo kupitia majadiliano tutapata ufumbuzi au mapendekezo ya hatua za kuchukua katika kuboresha masuala mbalimbali.
Ndugu washiriki;
Waandishi wa habari ni nyenzo muhimu sana ya utoaji wa taarifa kwa wananchi hasa kipindi hiki cha kampeni na uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Nitoe rai kwa waandishi wa habari kutekeleza majukumu yenu kwa kufuata sheria, kanuni, maadili na misingi ya uandishi wa habari. Nchi yetu ina vyombo vingi vya habari, vile vya magazeti ya kuchapisha, vyombo vya habari vya mtandano, Televiseni na radio. Mpaka sasa Tanzania ina jumla ya magazeti 179, Majarida mbalimbali 174, Vituo vya radio 247, vyombo vya habari kwa njia ya mtandao (online media) kwa ujumla ni 355 na vituo vya televisheni 68. Hii inafanya jumla ya vyombo vya habari vilivyosajiliwa nchini kufikia takribani 1023.
Ndugu washiriki;
Ni dhamira yangu ya dhati kuhakikisha tunafanya mageuzi kwenye sekta hii muhimu ya Habari, na tumeanza na kazi za kisera na kisheria. Kama nilivyoeleza hapo juu tuna jumla ya vyombo 1023 lakini nimedhamiria kuwafikia wadau wote, kwa kuanza na makundi na baadae kutembelea chombo kimoja kimoja cha habari kwa lengo la kuwasikiliza na kubadilishana mawazo na uzoefu ili sekta yetu iwe bora zaidi na yenye mchango mkubwa kwa Taifa. Nipende kuwafahamisha tu kwamba tarehe 21 mwezi huu, siku ya Alhamisi, saa 4 asubihi wiki hii nitakutana na Umoja wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRI) ambapo ndani yake kuna takribani taasisi 16 za kihabari (1. MCT, 2. TEF, 3. TAMWA, 4. MISA TANZANIA, 5. THRDC, 6. SIKIKA, 7. POLICY
FORUM, 8. LHRC, 9. JAMII FORUMS, 10. UTPC, 11. OJADACT, 12. TCID, 13. TADIO,
14. MOAT, 15. TWAWEZA na 16. TLS) na baadae nitaendelea kukutana na taasisi moja moja kama nilivyoeleza hapo awali, na chombo kimoja kimoja. inawezekana nisimalize vyote 1023 lakini taasisi zao zitawawakilisha.
Ndugu washiriki;
Kwa haya machache, naomba sasa nitamke kwamba Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Habari Kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 umefunguliwa rasmi.