Na Sabiha Khamis, Maelezo Zanzibar
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Dkt. Saada Mkuya Salum amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kufanyia kazi vikosi vya SMZ ili kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama nchini.
Akizungumza katika ufunguzi wa mahanga na ofisi za Kikosi cha Valantia (KVZ) kambi ya Mwanyanya Wilaya ya Magharib “A” ikiwa ni shamrashamra za kuelekea miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar amesema kufanya hivyo kutasaidia vikosi hivyo ikiwemo KVZ kuimarisha jukumu lao la msingi la kulinda raia na mali zao na kuzidisha doria katika maeneo hayo na nchi kwa ujumla.
“Kumekuwa kunajitokeza makundi hatarishi katika maeneo haya ya msitu kunakuwa na vijana watukutu ambao hufanya vitendo vya uhalifu na kuhatarisha maisha wa wakaazi wa maeneo ” amesema Dkt. Saada.
Alifahamisha kuwa Serikali itaendelea kuimarisha maslahi ya watendaji wa vikosi hivyo na kuwaejenga mazingira bora pamoja na kuvijengea uwezo vikosi hivyo juu ya dhana ya kujiendeleza kiuchumi ili kuleta maslahi na kupiga hatua za maendeleo ikiwa ni katika utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Ameeleza kuwa Vikosi hivyo vimekuwa vikifanya kazi nzuri kwa miaka mingi lakini katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya awamu ya nane chini ya Dkt. Mwinyi vikosi hiyvo vimefanya kazi nzuri zaidi katika kujiinua kichumi ikiwemo Kikosi cha Valantia (KVZ).
“Miaka yote vikosi hivi vimekuwa vikifanya vizuri katika majukumu yake lakini kwa miaka hii mitatu ya Dkt. Mwinyi vimefanya vizuri zaidi” alisema Waziri.
Hata hivyo amewasisitiza wapiganaji hao kuwa waaminifu katika kutunza siri ili kuepusha changamoto katika sehemu za kazi pamoja na kuandaa utaratibu mzuri wa kuwapa hamasa watoa taarifa ambao ni wananchi wanapotoa taarifa za kiusalama ambazo zisaidia kudhibiti vitendo viovu na kusisitiza kuwa na usiri mkubwa kwa watoa taarifa hao.
Vilevile amewashauri kikosi hicho kuanza kujenga majengo ya ghorofa kwani kila maendeleo yanapopatikana na idadi ya askari inaongezeka na kuzungusha ukuta katika eneo hilo ili kuliepisha uvamizi .
Akitoa taarifa ya kitaalamu kuhusu ujenzi wa mahanga na ofisi za KVZ kambi ya Mwanyanya Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya RaisTawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ Issa Mahfoudh Haji amesema zaidi ya Milioni 600 zimetumika kumlipa Mzabuni kwa ajili ya vifaa vya ujenzi huo.
Amesema ujenzi huo unahusisha majengo manne ikiwemo nyumba mbili za Maafisa, Hanga moja kwa ajili wa wapiganaji na Afisi moja kwa ajili ya kazi za utawala ambapo nguvu kazi ya kikosi cha KVZ ilitumika katika kukamilisha ujenzi.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaongeza ari na bidii ya utendaji kazi kwa maafisa na wapiganaji wa kikosi hicho sambamba kupunguza changamoto ya majengo ya kisasa ya kiutawala na malazi.
Kwa upande wake mkuu wa Kikosi cha Valantia (KVZ) L.T Kanal Said Shamhuna amesema kukamilika kwa mradi huo kutatoa huduma mbalimbali kwa jamii ikiwemo huduma za maji safi na salama, afya pamoja na huduma za ulinzi na usalama ambazo zitasaidia kutokomeza vitendo vya kihalifu pamoja na unyanyasaji wa kijinsia.
Amesema mradi wa ujenzi huo katika kambi ya Mwanyanya umekwenda sambamba na ujenzi wa majengo kama hayo katika kambi za Muyuni na Kikungwi zilizopo mkoa wa Kusini Unguja na Mto wa maji kwa Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Wziri wa Nchi (OR),fedha na mipango dkt.Saada Mkuya Salum akikagua Ofisi ya kikosi cha valantia Zanzibar kambi ya mwanyanya kabla ya kufungua mahanga na Ofisi hiyo katika shamrashamra za kutimiza miaka 60 ya Mapinduzi.
Waziri wa Nchi (OR),fedha na mipango dkt.Saada Mkuya Salum akikata utepe kuashiria ufunguzi wa mahanga na Ofisi ya Kikosi cha valantia (kvz) kambi ya mwanyanya ,mradi uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 600 katika shamrashamra za kutimiza miaka 60 ya Mapinduzi.
Waziri wa Nchi (OR),Fedha na Mipango dkt.Saada Mkuya Salum akikunjua kitambaa kuashiria UFUNGUZI wa Ofisi na mahanga ya kvz kambi ya mwanyanya katika shamrashamra za kutimiza miaka 60 ya Mapinduzi.
Waziri wa Nchi (OR),Fedha na Mipango dkt.Saada Mkuya Salum akihutubia mara baada ya kufungua Ofisi na mahanga ya Kikosi cha valantia kvz kambi ya mwanyanya katika shamrashamra za kutimiza miaka 60 ya Mapinduzi
Mkuu wa kikosi cha kvz luteni kanal Saidi Shamhuna akizungumza machache wakati wa ufunguzi wa mahanga na Ofisi za Kambi za Kvz Mwanyanya uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 600 katika shamrashamra za kutimiza miaka 60 ya Mapinduzi
PICHA NA FAUZIA MUSSA -MAELEZO ZANIBAR