Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Waziri wa Sheria na Katiba Dkt.Damas Ndumbaro amewashangaa baadhi ya wadhamini wa taasisi, zikiwemo za kidini, ambao hawatimizi majukumu yao kikamilifu na wanatumia mali za taasisi zao kwa maslahi binafsi.
“ Hivi karibuni, sisi sote ni mashahidi, kumekuwa wa ongezeko la migogoro katika taasisi mbalimbali nchini ambayo inasababishwa na mapungufu ya usimamizi wa wadhamini. Inashangaza kuona hali hii inajitokeza hata katika taasisi za kidini ambazo kikawaida zinatakiwa kuwa mfano wa kuigwa katika jamii,” alisikitika Dkt.Ndumbaro.
Akishiriki katika mkutano wa wajumbe wa bodi za wadhamini zilizomo mkoa wa Dar es Salaam uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere, waziri huyo alisema bado ipo changamoto ya wadhamini kutotimiza majukumu yao kikamilifu na wanatumia mali za taasisi kwa maslahi binafsi.
Ameeleza kwamba migogoro katika taasisi na jamii inatokana na baadhi ya wadhamini kufuja fedha na kutumia mali za taasisi kwa ubadhirifu.

“Migogoro na ubadhirifu katika taasisi za dini ni jambo linaloshusha imani ya wananchi kwenu, hivyo ni vema wadhamini mtafakari kwa kina na kuamue kubadilika,”
Hata hivyo alionya kuwa hatua stahiki zitachukuliwa kwa wale wote wanaokiuka misingi ya sheria katika utekelezaji wa majukumu yao.
Aliupongeza Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa kuandaa kikao kazi hicho kwa lengo la kuwakumbusha wadhamini hao majukumu yao na kuwajengea uwezo wajumbe wa bodi kwa kuwapa fursa ya kubadilishana uzoefu
Amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na taasisi zake imedhamiria kuimarisha usimamizi wa bodi za wadhamini kwa lengo la kupunguza migogoro na ubadhirifu katika taasisi zao.
Pamoja na mambo mengine, ameziagiza taasisi zote kufanya marejesho kila mwaka kama sheria inavyosema.
Pia amezitaka bodi zote za wadhamini kuhakikisha udhibirifu wa fedha na mali havitokei. Pia amezitaka taasisi kuhakikisha bodi zinapomaliza muda wake ufanyike uchaguzi na ameitaka RITA kuunda kikosi kazi kwa ajili ya kuzifuatilia utendaji wa taasisi.
Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa RITA, Dkt Amina Msengwa amewataka wajumbe wa Bodi za Wadhamini kuheshimu mali za taasisi kwani wao siyo wamiliki wa mali hizo.
“Tunaamini mafunzo haya yatasaidia kuwajengea uwezo na uelewa wa majukukumu yao sambamba na kuzisajijili bodi/taasisi zao kupitia mfumo wa e-RITA,” alisema Dkt Msengwa na kuongeza kuwa wajumbe wa bodi za udhamini wanapaswa kufanya kazi zao kwa weledi ma kwa kuzingatia sheria.
Kabidhi Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Bw. Frank Kanyusi, alisikitishwa na tabia ya bodi za wadhamini kutumia pesa nyingi za umma; fedha ambayo ingeumika kwenye mambo mengine ya kijamii.
“Usuluhisi wa migogoro inayotokea katika bodi za wadhamini imekuwa ukitumia fedha nyingi za umma bila sababu ya msingi.Hivyo, tumekutana leo kwa ajili ya kuwakumbusha wadhamini majukumu yao ili kupunguza au kumaliza kabisa changamoto za kiutendaji katika bodi zenu.” amesema.
Bw. Kanyusi amesema kuwa ofisi yake inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kwa lengo la kutatua migogoro inayojitokeza katika taasisi hiyo, ikiwa ni pamoja na kuunda kamati maalum za kuchunguza tuhuma mbalimbali zinazojitokeza.