Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damasi Ndumbaro, amehamasisha wananchi wa Manispaa ya Songea kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la wapiga kura.

Dkt. Ndumbaro ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea mjini ametoa hamasa hiyo leo katika vituo vya kujiandikisha kupiga kura vya Kata ya Lizaboni,Mji mwema,Matarawe pamoja na kata ya Bombambili katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma .

Waziri Dkt.Ndumbaro alijiandikisha katika kituo cha Chekechea kilichopo kata ya Mji Mwema ambapo alizungumza na wananchi na alisisitiza umuhimu wa ushiriki wa kila mmoja katika mchakato wa uchaguzi, pamoja na kuwataka vijana na wanawake muda wa kuchukuwa fomu utakapofika wajitokeze kuchukuwa fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wa Serikali za Mitaa.

Alisema kuwa ni haki na wajibu wa wananchi kushiriki katika kuunda mustakabali wa nchi yao na kujipatia viongozi watakao waongoza kwa misingi ya kufuata kanuni Sheria na taratibu zilizowekwa na si vinginevyo.

Waziri aliwataka wananchi kuchangamkia fursa hii kwa kujiandikisha ili waweze kushiriki katika uchaguzi wa viongozi watakaowakilisha maslahi yao.

Dkt. Ndumbaro, alitaja faida za kuwa na idadi kubwa ya wapiga kura, akisema kuwa inasaidia kuimarisha demokrasia na uwakilishi na kwamba ni wajibu wa viongozi wa mitaa na jamii kuhakikisha wanatoa elimu kuhusu umuhimu wa uchaguzi na kuhamasisha watu kujiandikisha.

” Nimekuja kuungana na wanamji mwema wenzangu na wanasongea kuja kujiandikisha katika daftari la wapiga kura wa uchaguzi wa serikali za mitaa ,nimekuja hapa mjimwema A ndiko nyumbani kwangu nyumbani kwa baba yangu na Mimi nimekuja kujiandikisha, zoezi hili ni la kikatiba, Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imesema kila raia ana haki ya kushiriki kwenye shughuli za kisiasa kwa maana ya kuchagua na kuchaguliwa.

“Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni uchaguzi muhimu sana sana kuliko uchaguzi Mkuu, maendeleo yanatokana na Serikali za Mitaa kila maendeleo mnayoyaona yanaanzia kwenye mtaa wanayajadili yanakwenda kwenye kata wanayajadili yakitoka kwenye kata yanakwenda kwenye halmashauri wanayajadili na baadae mimi nayachukuwa kama mbunge wenu na kuyapeleka taifani hivyo ukitaka maendeleo kwenye mtaa wako jiandikishe na ukapige kura “alisema Waziri Ndumbaro.

Alisema kuwa unapochagua kiongozi mzuri ndipo unapochaguwa maendeleo hautamlaumu Rais wa Jamuhuri ya Muungano Dkt Samia Suluhu Hassan wakati hamchagui viongozi kwenye Serikali za Mtaa hivyo zingatieni ya kwamba hili ni zoezi muhimu sana kwa mustakabali wa maendeleo ya Nchi yetu.

Kwa upande wake mmoja wa waandikishaji katika kituo cha chekechea kilichopo kata ya Mjimwema Zamda Mbaraka alisema kuwa wamepangiwa kuandikisha wananchi 3000 wa kata hiyo ambapo kwa siku wanatakiwa kuandikisha wananchi wasiopungua 295 wakati huo huo mtendaji wa kata ya Bombambili Hassan Mataja alisema kuwa kata yake amepangiwa kuandikisha wapiga kura 13270 ambapo amesema kuwa hadi jana ameandikisha Jumla ya wananchi 400 sawa na asilimia 38 na ana uhakika wa kuvuka lengo la idadi aliyopangiwa ya uandikishaji kwenye daftari la kupigia kura.

Please follow and like us:
Pin Share