Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt.Damas Ndumbaro amegawa vitabu vya Kiada vyenye thamani ya sh.miilioni 27,217,000 kwa wanafunzi wa shule ya sekondari ya wavulana (Songea boys)iliyopo katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Hafla ya ugawaji wa vitabu hivyo imefanyika jana katika viwanja vya shule hiyo ambapo vitabu zaidi ya 1000 vimekabidhiwa shuleni hapo kwa lengo la kukuza elimu na utamaduni miongoni mwa wanafunzi.
Alisema kuwa vitabu hivyo vitasaidia wanafunzi katika kuelewa vizuri masomo yao na kukuza maarifa yao kwa ujumla ikiwemo kuongezeka kwa ufaulu.
“Sisi Cosota kati ya majukumu ambayo tunayafanya ni pamoja na kutoa machapisho na kwanamna Serikali inavyowathamini wananchi wao inapaswa kuwaletea machapisho yao kwa watoto wao ambao ni wanafunzi ili waweze kuboresha elimu na kuwasaidia kujifunza kwa ufanisi zaidi.”alisema Waziri Dkt. Ndumbaro.
Waziri Dkt.Ndumbaro alisisitiza umuhimu wa kusema na kujifunza huku amewataka wanafunzi kutumia vitabu hivyo vizuri ili waweze ufaulu katika masomo yao.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Cosota Doreen Sinare amemshukuru Waziri wa utamaduni,sanaa na Michezo Dkt Ndumbaro, kwa kufanikisha zoezi hilo la ugawaji wa vitabu na kwamba vitabu vilivyogaiwa kwa wanafunzi wa shule ya sekondari ya Songea Boys ni vya Sayansi,hisabati,kiswahili na kingereza, historia na jiographia pamoja na vitabu vya tafsiri na fasihi.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Furaha Mwangakala alisema kuwa Dkt.Ndumbaro ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea mjini kitendo cha kugawa vitabu hivyo amefanya kwa vitendo kwa hiyo kuna kila namna ya kumpongeza na kama halmashauri ya manispaa ya Songea kwa kazi hiyo kubwa na yenye gharama kubwa ambayo itawasaidia sio kwa wanafunzi hao tu walio hapo mbali hata kwa kizazi vijavyo kwa kuwa wataendelea kuvisoma vitabu hivyo.