Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Deogratius Ndejembi ameupongeza Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kazi ambayo imekuwa ikifanya na kushuhudia kasi ya ukuaji wake.
Ndejembi ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya zaira katika Ofizi ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Makao Makuu na kuzungumza na menejimenti ya taasisi hiyo.
Amesema mfuko huo umekuwa ukikua vyema chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mkuu, Masha Mshomba ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani mwaka 2021 na kumteua Mkurugenzi Mkuu, Mfuko ulikuwa na thamani ya sh Trilioni 4.8, lakini ndani ya miaka mitatu ukuaji wa mfuko umefikia thamani ya sh Trilioni 8.1.
“Huu ni ukuaji wa hali ya juu, na ni mafanikio makubwa kwa Serikali ya Awamu ya Sita, ni mafanikio makubwa yaliyoletwa na Mkurugenzi wa Taasisi hii na Menejimenti yake kwa ujumla. Lakini ukiacha mafanikio haya kuna mambo ya msingi ambayo ni lazima tuyaone yakitokea,” amesema Ndejembi.
Amesema Serikali inataka kuona mfuko unaongeza nguvu ya huduma kwa mteja ambaye ni Mtanzania, yule ambaye anachangia kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, kwa kuhakikisha wanahudumiwa kwa wakati, na kero zao zozote ambazo wanaleta ziweze kuchukuliwa hatua mara moja.
Aidha amesisitiza Menejimenti ya NSSF
kuhakikisha inawekeza vizuri fedha za Mfuko ya Hifadhi ya jamii kwa uadilifu wa hali ya juu kwa kuwekeza kwenye miradi ambayo itaweza kurejesha ili kuweza kulipa mafao kwa wakati.
“Naomba muhakikishe miradi mnayohiyo iwezekeza inaweza kurejesha fedha na faida zaidi katika mifuko hii,” ameeleza Ndejembi.
Katika hatua nyingine Ndejembi amesema Serikali haitamvumilia mwajiri ambaye hatawasilisha michango ya watumishi kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa wakati.
“Wapo waajiri ambao tumeona wanafanya hivyo, sasa ile ni kumyima haki mwajiriwa katika eneo la kazi la kuweza kupata fedha yake, na kuna waajiri wengine, anakata fedha ya kwake, anakata fedha ya mwajiriwa na anatakiwa alete mchango wake yeye kama mwajiri, lakini anaoufikisha kwenye Mfuko wa NSSF ni ule aliomkata mwajiriwa peke yake lakini ule mchango wake yeye anaotakiwa kuuleta nao haufikishi,”amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NSSF,Masha Mshomba ameahidi yote waliyoelekezwa na kusisitizwa na Waziri Ndejembi watayatakeleza ikiwemo suala la kuboresha huduma kwa wateja.
Pia ameahidi watahakikisha wanashauriana na wadau wengine ili kufanikisha maboresho hayo.
Aidha amesema kuwa watahakikisha wanakuwa na usimamizi mzuri wa miradi wenye tija ambao utarejesha faida na kusaidia kulipa mafao kwa wastaafu.