Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ni miongoni mawaziri wachache wanaoheshimika nchini, kutokana na jitihada kubwa anazofanya katika kuwatumikia wananchi.

Watu wengi wamekuwa wakiunga mkono kasi ya utendaji wa waziri huyo, katika suala zima la kudhibiti udokozi na hujuma za mali za umma. Wengi tunamshukuru Mungu kwa kumrejeshea afya njema, baada ya kusumbuliwa na maradhi yaliyomlazimu kwenda kutibiwa nje ya nchi. Tunafurahi kuona amerudi kuendelea kulitumikia Taifa letu.


Hata hivyo, hivi karibuni, utendaji wa waziri huyo wa Wizara ya Uchukuzi umeingia dosari baada ya kuhamishia ofisi yake kanisani! Sijui kama mwenyewe amegundua kosa hilo. Dk. Mwakyembe anadaiwa kuhudhuria ibada katika Kanisa la Nduli mkoani Mbeya, na kutumia nafasi hiyo kulishambulia Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.


Inadaiwa waziri huyo alilituhumu jeshi hilo kwamba limekuwa na kigugumizi cha kuweka hadharani majina ya askari wake wanaotuhumiwa kuiba mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam. Tuhuma hizo zinawahusisha baadhi ya askari waliokuwa wakifanya doria katika bandari hiyo hivi karibuni. Kwamba walionekana wakitorosha mafuta yaliyoibwa na watu wasiojulikana.


Bila kujali alikuwa katika ibada, Dk. Mwakyembe anadaiwa kutoa tamko la kukusudia kulichongea jeshi hilo kwa uongozi wa juu serikalini (bila shaka kwa rais), kama uongozi wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam utashindwa kulishughulikia katika kipindi cha wiki mbili.


Kwamba uongozi wa jeshi hilo umeshindwa kuonesha dhamira ya kweli katika kuchukua hatua za kisheria dhidi ya askari wanaotuhumiwa kuiba mafuta bandarini.

 

Kauli hiyo ya Waziri Dk. Mwakyembe imewaacha midomo wazi watu wengi, kwa vile ameitoa katika sehemu isiyo rasmi na mwafaka, yaani ibadani. Mahali ambapo watu huenda kufanya kazi moja tu ya kumwabudu Mungu.

 

Kwa hakika waziri huyo ameteleza kutoa kauli hiyo kanisani ambako kwa kawaida waamini huweka kando masuala mengine yote na kujikita katika kazi moja ya kusali, kauli ambayo sasa imetia doa juhudi zake nzuri za kutetea maslahi ya umma kupitia maeneo yake ya uongozi.

 

Waswahili wanasema kuwa kosa moja hufuta mazuri 99 yaliyotekelezwa. Hilo linaweza kuwa kosa la kwanza linaloweza kufuta mazuri mengi yaliyofanywa na Dk. Mwakyembe tangu achaguliwe kuwa Mbunge wa Jimbo la Kyela, na baadaye kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Waziri wa Uchukuzi.


Kuna swali kuu la kujiuliza hapa. Kwanini Waziri Dk. Mwakyembe aliamua kutofuata itifaki ya serikali kwa kuwasiliana na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam, Suleiman Kova, kama kweli alitaka suala hilo lishughulikiwe haraka kisheria?

 

Lakini pia, kama waziri huyo alihisi na kuona Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam haoneshi nia ya kushughulikia suala hilo kwa uzito unaostahili, bado alikuwa na nafasi ya kuwasiliana moja kwa moja na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Said Mwema.

Kwa upande mwingine, waziri huyo hawezi kukwepa lawama kwamba alitumia muda wa ibada hiyo vibaya kwa kuzungumzia masuala ya ofisini kwake kinyume cha taratibu za serikali na Kanisa.

 

Siku zote ibada inapaswa kutawaliwa na sala/swala pamoja na maombi mbalimbali ya binadamu kwa Mwenyezi Mungu. Kinyume cha hapo ni kufuru, pengine hata mbele za Mwenyezi Mungu.

 

Pengine nia ya Dk. Mwakyembe ilikuwa kujipatia umaarufu wa kisiasa mbele ya waamini na uongozi wa Kanisa la Nduli kwamba ni waziri mwenye nguvu kubwa serikalini. Kweli ni kiongozi mwenye nguvu, lakini wengi tumeona kuwa alifanya kosa la kutoa maelekezo ya serikali kanisani.

 

Inawezekana pia Waziri Dk. Mwakyembe alikuwa na jazba na uchungu, baada ya kuambiwa askari polisi wenye dhamana ya kulinda usalama wa raia na mali zao wanashiriki kuhujumu usalama huo. Lakini bado alikuwa na uwezo wa kutumia angalau mkutano wa hadhara kutema nyongo hiyo badala ya kuitema kanisani.

 

Ni dhahiri kuwa kitendo hicho cha Dk. Mwakyembe kimekiuka moja kwa moja itifaki ya serikali na madhumuni ya Kanisa.


Wanasiasa na viongozi wa serikali akiwamo Dk. Mwakyembe wanapaswa kuheshimu nyumba za ibada, wakitambua kuwa ni sehemu maalumu kwa ajili ya binadamu kwenda kuungama dhambi na kuomba rehema za Mwenyezi Mungu juu ya masuala mbalimbali ya kidunia.

 

Ifike mahali madhehebu ya dini nayo yaangalie uwezekano wa kupiga marufuku matumizi mabaya ya ibada, vinginevyo yatajipunguzia kama si kujipotezea umaarufu kwa sababu tu baadhi ya viongozi wa kisiasa na serikali wanaamua kuyatumia kujipatia umaarufu binafsi.