Serikali imeweka zuio la matumizi ya fedha za kigeni katika manunuzi ya huduma na bidhaa mbalimbali nchini ili kulinda nguvu ya fedha ya Tanzania.
Hatua hii imekuja kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kuiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kudhibiti matumizi ya fedha za kigeni katika biashara na huduma hapa nchini ili kulinda nguvu ya fedha ya Tanzania na kukabiliana uhalifu wa kifedha.
Katika kutekeleza hatua hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, akizungumza na waandishi wa habari jana, Ijumaa, Disemba 29, alitoa maagizo ambayo yamelenga kuzuia matumizi ya fedha za kigeni hapa nchini.
“Bei zote hapa nchini zitangazwe kwa shilingi ya Tanzania. Na bei hizi zinajumuisha kodi ya nyumba za khi na maofisi, bei ya ardhi, gharama za elimu na afya, bei ya vyombo vya usafiri na vyombo vya klektroniki… kuanzia Januari tukikuta umetangaza biidhaa zako hizi kwa dola au Euro, sheria ina wewe,” amesema Waziri Mpango.
Kwa upande wa watalii na wageni kutoka nje ya nchi, Waziri Mpango ameeleza kuwa wanaruhusiwa kufanya manunuzi ya huduma na bidhaa kwa fedha za kigeni.
“Bei ambazo walengwa wke wakuu ni watalii, au ateja wasio wakazi, zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni. Bei hizi zinajumuisha gharama za usafirishaji kwenda nchi za nje kupitia Tanzania, gharama za mizigo bandarini kwenda nchi za nje, gharama za uwanja wa ndege na visa kwa wageni, lakini gharama za hoteli kwa watalii kutoka nje ya nchi,” amesema.
Aliongeza kuwa, wote watakaolipia huduma na bidhaa kwa fedha za kigeni, ni lazima watambuliwe kupitia vitambulisho vyao ikiwemo pasi za kusafiria.
“Walipaji wanaotumia fedha za kigeni, watambuliwe kwa vitambulisho vyao kama vile pasi za kusafiria na nyaraka za usajili kwa makampuni,” amesema Dk. Mpango.
Waziri Mpango amesisitiza kuwa viwango vya ubadilishaji wa fedha vitakavyotumika, viwekwe wazi na benki pamoja na maduka ya fedha peke yake ndiyo wanaoruhusiwa kupanga viwango hivyo kutokana na ushindani uliopo katika soko la fedha za kigeni.
“Viwango vya kubadilishana fedha vitakazotumika katika kuweka hizo bei katika sarafu mbili, viwekwe wazi na visizidi vile vya soko. Na ifahamike wazi ni mabenki na maduka ya fedha za kigeni peke yao ndiyo yanayoruhusiwa kupanga viwango vya kubadilishana fedha kutokana na ushindani katika soko la fedha za kigeni,” amesema.
Aidha Waziri mpango amesisitiza kuwa wanancwa Tanzania wasilazimishwe kulipia huduma au bidhaa yoyote kwa fedha za kigeni, na kuziagiza mamlaka husika kuwachukulia hatua kali za kisheria wote watakaobainika kuenda kinyume na maagizo hayo.
“Mkazi yeyote wa Tanzania asilazimishwe kulipia bidhaa au huduma yoyote hapa nchini kwa fedha za kigeni. Ninavitaka vyombo vya dola viwachukulie hatua za kisheria wale wote watakaobainika kukiuka maagizo ya serikali,” alisisitiza Dkt Mpango.