Waziri Mkuu wa Chad Succes Masra ametangaza kuwasilisha barua yake ya kujiuzulu Jumatano, ikiwa wiki kadhaa zimepita baada ya kushindwa na Mkuu wa Serikali ya Kijeshi Jenerali Mahamat Idriss Deby katika uchaguzi wa rais uliofanyika Mei 6, mwaka huu.
Masra mwenye miaka 40 ambaye ni mpinzani mkubwa wa serikali ya kijeshi, ambayo ilichukua madalaka mwezi Aprili 2021. Aliteuliwa kuwa waziri mkuu wa serikali ya mpito mwezi Januari, miezi minne kabla ya uchaguzi wa nchi hiyo.
“Nimewasilisha barua yangu ya kujiuzulu na ile ya serikali ya mpito, ambayo haikuwa na umuhimu lakini ni kwa mujibu wa katiba,” Masra ameandika katika ukurasa wake wa twitter.
Deby mwenye miaka 40, alitangazwa rais wa mpito mwezi Aprili 2021 na serikali ya kijeshi ya majenerali 15 baada ya baba yake, Rais Idriss Deby Itno, kuuawa kwa kupigwa risasi na waasi baada ya kukaa miaka 30 madarakani lakini Masra aliyapinga matokeo ya ushindi wa Deby.
Deby alishinda uchaguzi wa urais wa Mei 6 kwa asilimia 61 ya kura, kulingana na matokeo ya mwisho.
Masra, katika uchaguzi huo alipata asilimia 18.5 ya kura lakini akapinga matokeo hayo.
Alidai ushindi katika uchaguzi huo, ambao chama chake kiliita “kinyago” na mashirika ya kutetea haki za kimataifa yalisema hautakuwa wa kuaminika wala wa haki.
Baraza la Katiba baadaye lilimthibitisha Deby kama mshindi, na Masra alikubali uamuzi wake, akisema hakuna njia nyingine za kisheria za kupinga matokeo.
Kura zilizopigwa siku ya Jumatatu ya wiki mbili zilizopita zililenga kuumaliza utawala wa miaka mitatu wa kijeshi katika nchi hiyo inayozalisha mafuta ya kanda ya Sahel iliyopo kwenye mapambano na makundi ya itikadi kali za dini ya kiislamu.