Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi Siku ya Kilele cha Maadhimisho ya UKIMWI Duniani itakayofanyika kitaifa December 1 mwaka huu mkoani Morogogo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera, Bunge na Uratibu Jenister Mhagama ameeleza hayo leo November 14,2023 Jijini hapa kwenye mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya siku ya ukimwi Duniani .
Ameeleza kuwa Wadau wa Kitaifa na Kimataifa chini ya uratibu wa TACAIDS wanaendelea na maandalizi kwa ajili ya
kutoa huduma muhimu wakati wa Maadhimisho na kwamba kwa kawaida
siku hiyo huadhimishwa ndani ya wiki moja ambapo shughuli mbalimbali zinazohusu Utoaji wa taarifa za udhibiti wa VVU na UKIMWI zitafanyika kuanzia tarahe 24 Novemba, 2023 hadi siku ya kilele ya tarehe 1.disemba 2023.
“Mikoa yote nchini imeelekezwa kuandaa na kuadhimisha siku hii, Kupitia Ofisi ya
Rais TAMISEMI, natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa wote nchini kusimamia utekelezaji wa shughuli hii kwa kushirikiana na wadau wa kudhibiti VVU na UKIMWI walioko kwenye Mikoa yao, ” amesema
Amefafanua kuwa huduma za VVU na UKIMWI zinaendelea kutolewa kwa kiwango cha kuridhisha na kwamba upimaji wa
hiari na utoaji wa dawa za ARV umekuwa na mafanikio makubwa kwa kuzingatia kigezo cha malengo ya 95 – 95 – 95.
Amesema,”Hii ina maana kuwa Asilimia 95 ya watu walio na maambukizi ya VVU
wawe wametambua hali zao, Asilimia 95 ya wale wanaotambua kuwa wanaishi na VVU wawe wanatumia dawa za ARV na
asilimia 95 ya wale wanaotumia ARV wawe wamefubaza VVU mwilini,”amesema na kuongeza;
“Kipimo cha utendaji wetu katika kufikia malengo hayo tutakipata tarehe 1 Desemba 2023 baada ya kutangazwa na mgeni rasmi kufuatia kukamilika kwa Utafiti wa Viashiria vya VVU na UKIMWI (Tanzania AIDS Impact Survey – THIS) wa mwaka 2022/23 ambao utatoa picha ya hali halisi ilivyo sasa.
Ndugu Wanahabari, natoa wito kwa wananchi na wadau wote kushirikiana katika kupanga na kutekeleza shughuli za kudhibiti VVU na UKIMWI kwa kuzingatia vipaumbele na mahitaji ya mahali walipo, “amesema.
Waziri huyo pia ameyataja maeneo yanayohitaji msukumo zaidi katika mapambano hayo kuwa ni pamoja na watoto na vijana na kwamba kwa kufanikiwa katika hilo Tanzania itakuwa imetimiza ndoto ya kumaliza VVU na UKIMWI ifikapo mwaka 2030.
Amesema Serikali inaongeza msukumo na
vipaumbele kuimarisha afua za VVU na UKIMWI kwa vijana kwani takwimu zilizopo zinaonesha kuwa, kundi la vijana wa umri wa miaka 15 hadi 24 linachangia maambukizi
mapya ya VVU kwa asilimia 40 na hivyo kulifanya kundi hili kuwa keenye hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi ya VVU.
“Maadhimisho ya mwaka huu yanatoa
kipaumbele pia kwa vijana kushiriki kikamilifu kwenye majukwaa ya matukio yalioandaliwa kwenye maadhimisho haya kote
chini, matukio yaliyopangwa kufanyika katika maadhimisho ya siku hiyo ni maonesho ya Shughuli za Wadau wa kudhibiti VVU na
UKIMWI nchini yatakayoanza tarehe 24 Novemba, 2023 hadi Desemba 12023;”amefafanua
Kwa upande wake Meneja Mpango wa Taifa wa kudhibiti Ukimwi kutoka Wizara ya Afya Dkt. Anath Rwebemberwa amesema wizara imekuja na mkakati wa kusambaza Kondomu ili kudhibiti watu kuchukua Kondomu nyingi badala ya kuchukua Mbili au tatu kwa matumizi yake.
“Sasa hivi tunaenda kupanga usambazaji mwingine mpya wa usambazaji wa Kondomu mana mfumo ambao uliopo Sasa unakuta mtu anachukua Kondomu nyingi Kwa matumizi yake na hata kuziuza,hivyo utaratibu tutakaokuja nao utaruhusu mtu kuchukua kondomu tatu tu” amesema.
Naye Dkt. Jerome Kamwela, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, amesema matokeo ya tiba yanaonesha kuwa wanaume ni wavivu kwenda kupata huduma ya Tiba.
“Wanaume ndiyo wanakufa zaidi kwa ugonjwa wa ukimwi kuliko wanawake kwa sababu hawapimi na hawaendi Kwenye huduma, hivyo wanaume jitikezeni kupima ili mjue hali zenu” amesema
Maadhimisho ya siku ya ukimwi Duniani kwa mwaka huu 2023 yanaongozwa na kauli mbiu isemayo “Jamii Iongoze Kutokomeza UKIMWI” ambapo maadhimisho hayo yataadhimishwa ndani ya wiki moja ambapo shughuli mbalimbali zinazohusu Utoaji wa taarifa za udhibiti wa VVU na UKIMWI na huduma ya Upimaji wa Hiari wa VVU zitafanyika kuanzia tarahe 24 Novemba, 2023 hadi siku ya kilele ya tarehe 1.disemba 2023.
Hayo yanajiri baada ya Serikali kukamilisha kutoa taarifa ya Utafiti wa viashiria na Matokeo ya VVU na UKIMWI Nchini kwa Mwaka 2022/2023 huku takwimu za Utafiti huo zikitarajiwa kutolewa rasmi Desemba Mosi Mwaka huu Mkoani Morogoro katika Maashimisho hayo.
Aisha Utafiti huo unaonesha Tanzania imepata matokeo chanya kutokana na idadi ya Maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi kuendelea kupungua ikilinganishwa na Utafiti uliofanywa 2016/2017.