Mheshimiwa Waziri Mkuu, naandika barua hii mahususi kwako kuhusu Kijiji cha Butiama ambako ndiko Makao Makuu ya Wilaya ya Butiama.

Uamuzi wa kuifanya Butiama kuwa Makao Makuu ya Wilaya ya Butiama ni utekelezaji wa uamuzi wa kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM kilichoketi hapa kijijini mwaka 2008 chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa wakati huo, Rais Jakaya Kikwete.

Uamuzi wa NEC ulilenga kuhitimisha mvutano usiokuwa na tija uliotaka makao makuu yawe Kiabakari. Mvutano huo bado upo. Mapambano yameendelea kwa muda wote huo kuhakikisha Butiama inabaki jina tu.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, njama za kuidhoofisha Butiama ziko wazi kabisa, si za kificho tena. Nadiriki kukuambia kuwa Butiama ni makao makuu ya wilaya ‘hewa’.

Ingawa wilaya nzima ya Butiama imejaa shida, naomba nitoea mifano michache inayohusu Kijiji cha Butiama. Kijiji hiki japo kinasemwa kuwa ndiyo makao makuu ya wilaya, barabara zake ni mbaya. Zinachongwa zinazozunguka kwa Baba wa Taifa, tena wakati wa ujio wa wageni. Mahali ambako ni makao makuu ya wilaya kwa maana ya ofisi za DC na za mkurugenzi yanaweza kuwa hafifu.

Butiama hatuna stendi ya mabasi. Butiama hatuna soko. Butiama hatuna maji. Butiama hospitalini tunapimwa na kuambiwa hatuna magonjwa, lakini tukienda hospitali nyingine ugonjwa unaonekana.

Ujenzi wa Makao Makuu ya Wilaya na Halmashauri ya Wilaya ya Butiama umekwama. Fedha zimetafunwa mchana kweupe. Hakuna kinachoendelea. Usambazaji umeme wa REA Butiama ni wa ujanja ujanja, kwa maana kuna nyumba na maeneo yanakwepwa. Watoto katika shule za msingi na moja ya sekondari wanaketi chini na wengine wanasomea chini ya miti. Tunajiuliza, tumeikosea nini serikali yetu?

Mheshimiwa Waziri Mkuu, mbaya zaidi, fedha zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za polisi. Ajabu, watu wa Ardhi hapa Butiama wamewanyima polisi kiwanja wakidai kuwa eneo lililotengwa kujengwa mji bado wenyewe hawajalipwa fidia.

Matokeo ya uamuzi huu, nyumba zaidi ya sita sasa zinajengwa Kiabakari! Kwanini nyumba zisijengwe Butiama ambako ndiko makao makuu ya wilaya? Kama ni upimaji, kwanini TAMISEMI hawaleti fungu – miaka 10 sasa- ili fidia zilipwe na viwanja vipimwe? Nini kinachelewesha haya mambo? Kwanini Butiama ijengwe ki-Manzese au ki-Tandale?

Pili, kuna taarifa za uhakika kuwa TANESCO nao wanataka kujenga ofisi zao, lakini zinajengwa Kiabakari! Kuna siri gani nyuma ya mpango huu? Kwanini miradi yote hii iwe nje ya Butiama? Kuna maana gani ya kuwa na makao makuu yasiyokuwa na huduma zote muhimu? Huku ndiko kumuenzi Baba wa Taifa?

Mheshimiwa Waziri Mkuu, wanaosema Butiama hakuna ardhi kwa ujenzi wa ofisi ni waongo. Kuna eneo kubwa lililokuwa la kijiji kabla ya kutwaliwa na serikali. Hata ujenzi wa makao makuu ya nchi unawezekana.

Mwisho, tunaomba Butiama tutendewe haki kama wanavyotendewa Watanzania wa maeneo mengine. Tunaomba vitu vyote nilivyovitaja vijengwe Butiama, isipokuwa miundombinu kama ya uwanja wa ndege na mingine mikubwa ijengwe maeneo yanayozunguka Butiama.

Asante sana.

Mwanakijiji,

Butiama.