Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameitembelea Timu ya Taifa ya Tanzania ya Mpira wa Miguu (Taifa Stars) inayofanya mazoezi kwenye uwanja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jijini Dar es Salaam na kusema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ana matumaini makubwa kuwa timu hiyo itafanya vizuri kwenye michezo yote miwili.

Majaliwa ameyasema hayo leo Jumatatu, Oktoba 07, 2024 alipoongea na Wachezaji, benchi la ufundi pamoja na viongozi wakiwa katika maandalizi ya michezo miwili ya kufuzu michuano ya AFCON 2025 dhidi ya Congo itakayochezwa Oktoba 10 na 15, 2024.

“Kila mmoja aone ana jukumu kubwa, kwako wewe mwenyewe na kwa Nchi yako, Rais Dkt. Samia anawatakia kila la kheri na alichofanya ametoa usafiri wa uhakika wa ndege itakayowapeleka Congo kwa ajili ya mchezo wa Oktoba 10, 2024, hili ni jambo kubwa”

Waziri Mkuu amesema kuwa kwa jitihada za Rais Dkt. Samia amefanikiwa kushawishi mashirikisho ya mpira wa miguu ya Afrika na FIFA ili kuiona Tanzania ni nchi ambayo imeamua kuboresha viwango vya michezo ikiwemo mpira wa miguu ambapo tayari tumeanza kuona heshima tunayoipata ya kuwa wenyeji wa baadhi ya mashindano ikiwemo CHAN.