WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amechukizwa na biashara za magendo zinazoendelea katika wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera, hivyo amewataka viongozi wa wilaya hiyo wajipime wenyewe.
Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Kagera Bw. Adam Ntogha kumsimamisha kazi Afisa wa Forodha katika mpaka wa Mulongo Bw. Peter Mtei kwa tuhuma za kujihusisha na biashara za magendo.
Ametoa agizo hilo jana (Jumanne, Oktoba 9, 2018) wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa Kagera katika kikao cha majumuisho ya ziara yake ya kikazi ya siku nne mkoani hapa kilichofanyika mjini Bukoba.
“Biashara za magendo zinafanyika bila ya wao kuchukua hatua, mnatia aibu yaani hakuna kazi inayofanyika. Viongozi wa wilaya ya Kyerwa mjipime wenyewe, mialo mingi katika wilaya yenu inatumika kwa biashara ya magendo na butura.”
Waziri Mkuu aliongeza kuwa katika mwalo wa Mulongo ulipo kwenye eneo ambalo Tanzania inapakana na nchi za Uganda na Rwanda, biashara za magendo na butura zinafanyika na hakuna kiongozi wanaochukua hatua.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimtaka Meneja wa TRA asiwahamishe watumishi wabovu kutoka kituo kimoja cha forodha na kuwapeleka kingine kwa kuwa huko wanakowapeleka wanakwenda kuendeleza biashara za magendo na kuikosesha Serikali mapato.
Alitolea mfano mtumishi wa mamlaka hiyo Bw. Mtei ambaye alihamishiwa kituo cha Mulongo akitokea kwenye kituo cha Mtukura kilichopo katika mpaka wa Tanzania na Uganda kwa tuhuma za kuchua rushwa na kushirikiana na wafanyabiashara wa burura.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema mtumishi huyo tayari alishapewa barua ya uhamisho kwenda katika kituo cha forodha cha Rusumo miezi minne iliyopita hadi sasa hajahama na anaendelea na biashara za magendo ambapo Agosti 5, mwaka huu anadaiwa kupitisha mzigo wa magendo uliobebwa kwenye gari aina ya fuso yenye za usajili T 957 AXF mali ya Erasto Muga.
“Meneja TRA msimamishe kazi Bw. Mtei leo (jana) hatuwezi kuwa na watumishi wabovu alafu nyie mnawahamisha vituo ili wakaendelee kuharibu eneo lingine. Mnajua mkakati wa Serikali hii ni kudhibiti rushwa hivyo hatuwezi kuvumilia suala hili.”
Kadhalika, Waziri Mkuu alimuagiza Meneja wa TRA wa mkoa wa Kagera Bw. Ntogha afanye ukaguzi kwenye vituo vyote vya forodha katika mkoa huo pamoja na kuongeza idadi ya watumishi na kudhibiti vitendo vya rushwa.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, SEPTEMBA 10, 2018.