Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali waweke msisitizo katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi na kuhamasisha zaidi upatikanaji wa masoko wa bidhaa za ndani na uwekezaji.

Amesema kuwa maboresho ya sera na mfumo wa uwekezaji uliofanywa na Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umesaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini.

Waziri Mkuu amesema hayo leo Septemba 19, 2022 alipokutana na mabalozi hao ofisini kwake Bungeni jijini Dodoma. Mabalozi aliokutana nao ni Balozi Caroline Chipeta (Uholanzi), Balozi Simon Sirro (Zimbabwe) na Balozi Luteni Jenerali Mathew Mkingule (Zambia),

Amesema Tanzania inahitaji wawekezaji makini watakowekeza kwenye sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, madini na maliasili. “Tunataka uwekezaji wenye tija ili kuimarisha uchumi wetu, pia tunataka wawekezaji watakaozalisha bidhaa hapa nchini kwa kutumia malighafi zetu.”

“Nchi yetu ni moja kati ya mataifa ambayo jiografia yake imekaa kimkakati, tuna masoko kutoka jumuiya mbalimbali ikiwemo SADC na EAC, hata mazingira yetu ya uwekezaji ni mazuri, tunazo ndege, bandari na sasa tunaendelea kufanya maboresho makubwa kwenye sekta ya nishati.”

Aidha,Majaliwa amewataka mabalozi hao kuandaa makongamano na vikao vya pamoja vya kibiashara kati ya wafanyabiashara wa nchi wanazoziwakilisha na sekta binafsi wa nchini Tanzania.

“Nendeni mkatafute masoko ya bidhaa zetu za ndani, shirikini kwenye maonesho yanayoandaliwa ili mtangaze bidhaa zetu, tunataka wakulima wetu wanufaike kwa kupata masoko kutoka kwenye nchi mnazokwenda” amesema.

Pia, amewasisitiza mabalozi hao wahakikishe wanalinda taswira ya Tanzania katika nchi uwakilishi sambamba na kujielekeza katika kuvutia watalii na kuwasaidia wafanyabiashara wa Kitanzania kufanya biashara nje.

Pia, Waziri Mkuu amewataka mabalozi hao wakajifunze teknolojia mpya na kuona namna inavyoweza kuisaidia Tanzania. “Suala hili linaenda sambamba na kutafuta fursa za masomo kwa vijana wetu katika nchi mnazokwenda.”

Waziri Mkuu amesema mabalozi hao wanatakiwa kuitangaza lugha ya Kiswahili. “Naamini mtatumia ushawishi wenu kukitangaza Kiswahili, angalieni namna ya kuanzisha madarasa ya lugha ya Kiswahili.”

Akizungumza kwa niaba ya mabalozi wenzake, Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Balozi Simon Sirro amesema kuwa kutokana na imani kuwa walioneshwa na Rais Samia watakwenda kufanya kazi na kuhakikisha nchi inanufaika na uwakilishi wao.