Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezielekeza halmashauri zote nchini zihakikishe maeneo yote yanayotwaliwa kutoka kwa wananchi yanalipiwa fidia kwa wakati ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza siku za usoni.

Amesema kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi kwenye maeneo mbalimbali nchini yakiwemo na ya jiji la Dodoma ya kutolipwa fidia baada ya maeneo yao kutwaliwa na halmashauri ya jiji.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Jumatano, Juni 28, 2023 wakati akitoa hoja ya kuahirisha Mkutano wa 11 wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mkutano huo umeahirishwa hadi Agosti 29 mwaka huu.

Amesema mahitaji ya uendelezaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii ikiwemo kuanzisha makazi yameendelea kuongezeka. “Ongezeko hilo ni muhimu likazingatiwa katika upangaji wa miji yetu hapa nchini.”

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amezielekeza halmashauri zote kupima maeneo kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na kijamii ikiwemo viwanja kwa ajili ya makazi badala ya kuacha wananchi kujenga kiholela.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amewaelekeza Maafisa Masuuli waimarishe usimamizi wa matumizi ya fedha za umma na kutekeleza kikamilifu Mpango wa Bajeti ya Mwaka 2023/2024.

Pia, Waziri Mkuu amezitaka Wizara na Taasisi za Serikali zifanye vikao kwa njia ya mtandao bila kuathiri tija ili kupunguza matumizi makubwa ya fedha za umma na gharama zisizo za lazima za uendeshaji wa vikao vya Serikali.

“Watendaji wa Serikali, imarisheni ukusanyaji wa mapato na kufanya matumizi kwa kuzingatia maeneo ya vipaumbele kwa mwaka 2023/2024 sambamba na kubuni vyanzo vipya vya mapato.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwataka watendaji wa Serikali wazingatie kanuni, sheria na taratibu katika manunuzi na matumizi ya fedha za umma ili kufikia shabaha na malengo ya uchumi.