Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameupongeza uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kuboresha huduma na mazingira ya hospitali hiyo.
Majaliwa ameyasema hayo leo alipotembelea Hospitali hiyo kumjulia hali ndugu yake aliyelazwa hapo ambaye anaendelea vizuri na kupata fursa ya kuwasalimia wagonjwa wengine.
“Nimefurahishwa sana jinsi mlivyoboresha huduma, wakati napita kusalimia baadhi ya wagonjwa wamenieleza kuridhishwa na huduma wanazopatiwa, hii inatia moyo sana.
“Nimefurahishwa na uboreshaji wa mwonekano wa Hospitali, mazingira, majengo na hii ndio Hospitali ya Taifa Muhimbili tunayoitaka” amesema Majaliwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Mohamed Janabi amemhakikishia Majaliwa kuwa menejimenti itaendelea kuimarisha huduma zake katika nyanja mbalimbali.