Waandamanaji wamempiga kwa yai Waziri Mkuu wa Australia, Scott Morrison.

Mkasa huo dhidi ya waziri mkuu ulitokea wakati wa mkutano wa kampeni Jumanne wiki iliyopita, bila kusita, walimtandika yai la kichwa. Vipande vya video vya tukio hilo vilionyeshwa kwenye televisheni za nchi hiyo.

Walinzi wa waziri mkuu huyo mara baada ya kitendo hicho, haraka sana, wakamdaka mwanamke mmoja miongoni mwa waandamanaji, na kuondoka naye.

Morrison alionekana akifuta kichwa chake mara baada ya kupigwa kwa yai hilo na kisha kumsaidia mwanamke mmoja mzee aliyesukumwa sakafuni wakati wa mvurugano huo.

“Tutasimama pamoja dhidi ya wakora, iwe ni hao wanahakarati wasio na heshima wala utu kwa yeyote au vikundi vya wahuni,” amesema Morrison kupitia ujumbe wake kwa njia ya mtandao wa twitter.

Tukio hilo limetokea wakati wa ziara ya waziri mkuu huyo huko Albury, jimbo lililoko New South Wales.

Mwanamke aliyevurumisha yai hilo kwa waziri mkuu baadaye aliwaambia waandishi wa habari kwamba, kitendo chake hicho “kinazungumza” chenyewe, akirejea yanayoendelea Kisiwa cha Manus, Papua New Guinea, ambako Australia imewashikilia wakimbizi kadhaa kwa mujibu wa mwanahabari kutoka gazeti moja la Australia.

Mwezi Machi mwaka huu kijana mmoja alimpiga kwa yai kichwani mbunge mmoja wa Australia kutokana na misimamo yake juu ya wahamiaji.