WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemaliza mgogoro wa matumizi ya pori tengefu la Loliondo ambao umedumu kwa takriban miaka 26.
Hatma hiyo imefikiwa jana (Jumatano, Desemba 6, 2017) kwenye kikao kilichoitishwa na Waziri Mkuu ofisini kwake Mlimwa, Manispaa ya Dodoma ili kutoa mrejesho uliofikiwa na Serikali kuhusu utatuzi wa mgogoro huo baada ya kupokea taarifa ya Kamati ya Uchunguzi.
Waziri Mkuu alisema Serikali imekubali mapendekezo ya kuunda chombo maalum kitakachosimamia eneo la Loliondo ili kunusuru ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti na kulinda mazingira na eneo mahsusi la mazalia ya wanyamapori, mapito na vyanzo vya maji.
“Baada ya kupitia mifumo mbalimbali, timu ya wataalam ilipendekeza kuwa utumike mfumo maalum utakaounda chombo maalum, kwa kuwa una maslahi mapana kwa pande zote husika na unalenga kuleta amani na kufikia lengo la kuwa na uhifadhi endelevu katika eneo la Loliondo,” alisema.
Waziri Mkuu aliiagiza Wizara ya Maliasili iandae muswada wa kutunga sheria mahsusi ya kuwa na chombo maalum au mamlaka ya kusimamia eneo la Loliondo ili kunusuru ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti pamoja na kulinda mazingira na eneo mahsusi la mazalia ya wanyamapori, mapito na vyanzo vya maji kwa ajili ya ustawi wa hifadhi muhimu zenye maliasili na rasilimali za Taifa kwa manufaa ya wananchi wenyewe na Taifa kwa ujumla.
“Sheria itakayotungwa ihakikishe inawekewa masharti yanayozingatia maslahi ya jamii iliyopo katika eneo la Loliondo, mila zao na desturi zao pamoja na mahusiano yao na matumizi ya ardhi,” alisisitiza Waziri Mkuu na kushangiliwa na wajumbe zaidi ya 60 waliohudhuria kikao hicho.
Vilevile, Waziri Mkuu aliiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii iandae waraka maalum utakaowasilishwa Serikalini kupitia Baraza la Mawaziri kuhusu umuhimu wa kutunga sheria mahsusi ya eneo la Loliondo.
Alisema kuna ulazima wa kushirikisha wadau wote mara baada ya rasimu ya kwanza kukamilika ili wadau waipitie kwanza. Alisisitiza rasimu ya pili iwe imefanyiwa mapitio na kukamilika ifikapo Februari au Machi, 2018 ili mahitaji ya fedha yaingizwe kwenye mchakato wa Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2018/2019.
Aliwataka Waheshimiwa Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Wizara za Kisekta zinazohusika na mgogoro wa matumizi ya ardhi ya Pori Tengefu la Loliondo wafanye ziara ya kutembelea eneo hilo ili wawe na uelewa mpana kuhusu changamoto za kisekta zilizopo katika eneo husika.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Mawaziri wa Maliasili na Utalii; TAMISEMI; Ardhi na Maendeleo na Makazi; Naibu Mawaziri wa Kilimo; Maji; Mifugo na Uvuvi na Elimu na Mafuzo. Pia kilihudhuriwa na wakuu wa taasisi za Serikali, wawekezaji walioko Loliondo, uongozi wa mkoa wa Arusha, madiwani na wananchi kutoka Loliondo.
Desemba 2016, Waziri Mkuu alifanya ziara ya kikazi wilayani Ngorongoro ambako alipokea taarifa ya kuwepo mgogoro wa matumizi ya ardhi katika Pori Tengefu la Loliondo. Januari 2017, aliunda Kamati ya Uchunguzi iliyokuwa na wajumbe 27 ambayo iliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo.
Washiriki wa kikao hicho waliopata fursa ya kutoa maoni, walipongeza uamuzi wa Serikali ya awamu ya tano wa kuwashirikisha wananchi hadi ngazi ya chini katika kutafuta suluhu la mgogoro huo.
Akichangia kwa niaba ya NGOs, Mkurugenzi wa taasisi isiyo ya Kiserikali ya Pastoralist Women Council, Bi. Manda Neritiko aliishukuru Serikali kwa kuwashirikisha wananchi kutafuta suluhu ya mgogoro huo, hatua ambayo alisema haijawahi kufanyika miaka yote ya nyuma.
“Huko nyuma tulikuwa tukipewa maagizo tu, Serikali imeamua hivi, Serikai imesema vile, lakini kwa awamu hii, tumeweza kuitwa kwenye vikao mbalimbali na kutoa maoni yetu na hata kupewa mrejesho,” alisema.
Aliomba hata katika chombo kipya kitakachoundwa, kuwe na uwakilishi wa wananchi kutoka ngazi ya chini ili waweze kushiriki kikamilifu katika kupanga namna bora ya kuendeleza eneo hilo.
Kwa upande wa wawekezaji, Bw. Scott Tineja Mollel kutoka kampuni ya AndBeyond Tanzania, alisema wao kama wawekezaji wanataka kuhakikishiwa kuwepo kwa utalii wa kesho. “Hatuwezi kuwa na utalii wa kesho kama hatutunzi mazingira ya sasa,” alisema.