Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Machi 29, 2025 amefanya ukaguzi wa viwanja vitakavyotumiwa kufanyia mazoezi na timu zitakazo shiriki michuano ya CHAN Agosti 2025 na AFCON 2027 kwa Ushirikiano na nchi za Kenya na Uganda.

Baada ya ukaguzi huo Mheshimiwa Majaliwa amewaagiza Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, na Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF) kufanya tathmini ya kazi ya ujenzi na ukarabati wa viwanja vya mazoezi vitakavyotumika kwenye michuano hiyo.

Ametoa maelekezo hayo leo baada ya kupokea maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa SUMA JKT, Brigedia Jenerali Petro Ngata ambaye ndiyo wakandarasi wa mradi huo.

Amesema ni vyema sasa ufuatiliaji wa karibu wa kila hatua za ujenzi na ukarabati ukafanyika ikiwa ni pamoja na ukaguzi wa vifaa vyote ambavyo Mkurugenzi huyo amesema tayari vimenunuliwa na viko Stoo.

“Ndani ya siku tatu hizi fanyeni tathmini mkutane na Mkandarasi na tembeleeni stoo na kuhakiki vifaa vyote ambavyo amesema vipo na muwasilishe taarifa kwangu tarehe 1 Aprili 2025.

Mkurugenzi huyo alimueleza Waziri Mkuu kuwa kwa ujumla ujenzi na ukarabati umefikia asilimia 80 ya kazi kwa viwanja vyote ambavyo ni pamoja na ujezi wa sehemu ya kuchezea (pitch) vyumba ya wachezaji (dressing rooms) pamoja na majukwaa.

Mheshimiwa Majaliwa alikagua viwanja vya Gymkhana, Meja Generali Isamunyo na kiwanja cha Chuo cha Sheria(Law School ) kilichopo Simu 2000 Ubungo.

Michuano ya CHAN 2025 inayoshirikisha wachezaji wa ndani inatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 2 hadi 30 Agosti 2025 baada ya kuahirishwa mwaka 2024, Vilevile michuano ya Afcon inatarajiwa kufanyika mwaka 2027.