WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Mawaziri wote, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa na Wilaya na Wakurugenzi watoe taarifa za fedha za miradi ya maendeleo kwa wananchi badala ya kusubiri ziara za viongozi wakuu.
Ametoa agizo hilo jana (Jumamosi, Januari 6, 2018) wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa kwenye kikao kilichofanyika hoteli ya Mt. Vicent, mjini Mbamba Bay, wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.
“Kuanzia sasa ninaagiza, viongozi wote wa ngazi za juu wakiwemo Mawaziri hadi Wakurugenzi na hata ninyi wakuu wa idara mnawajibika kutoa taarifa za fedha tunazopeleka kwenye miradi kwa sababu wananchi wana haki ya kujua utekelezaji wa ahadi za Serikali,” alisema.
Alisema kila wanapoenda kwenye ziara ya kikazi vijijini, waelezee thamani za kazi zilizofanyika na waeleze ni lini miradi hiyo itakamilika.
“Mnapopata fursa ya kupanda jukwaani, tumieni wasaa huo kueleza kazi kubwa ambazo zimefanywa na Serikali. Elezeni Serikali imeleta fedha kiasi gani, kwa ajili ya kitu gani na kwa kufanya hivyo, mtasaidia kutoa taarifa za utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa kampeni,” alisema.
Alisema wananchi wana haki ya kupatiwa taarifa za utendaji wa Serikali yao na akawataka viongozi hao wasisubiri ziara za viongozi wa kitaifa. “Nendeni mkaongee na wananchi, msiwaachie Wakuu wa Wilaya au Wabunge peke yao ndiyo waseme na wananchi,” alisema.
Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma kwa kukagua kituo cha kufua umeme kilichopo Unangwa, kuweka jiwe la msingi la ofisi ya TANESCO, kuzungumza na wananchi na kisha kuzungumza na watumishi wa Halmashauri ya Songea.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JANUARI 7, 2018.