Na Isri Mohamed
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa maagizo kwa Jeshi la Polisi kumkamata na kumuhoji mfanyabiashara Niffer ili aeleze ni nani aliyempa kibali cha kuchangisha fedha kwa ajili ya wahanga wa ajali ya Ghorofa lililoporomoka katika soko la Kariakoo.
Waziri Mkuu ameyasema hayo alipofika kutazama zoezi la uokoaji linavyoendelea mapema leo asubuhi.
“Tumeona kuna watu wanaanza kuchangisha changisha huko pembeni, wanasema michango kwa ajili ya waathirika wa kariakoo, serikali imeendelea kupokea kwa watu wema wakileta misaada yao hapa, na walichokuwa wanaleta hapa ni maji, vyakula, biskuti kwa ajili ya waokoaji hatujaruhusu mtu mwingine yeyote huko nje kuanza kuchangisha Watanzania kwa ajili ya tatizo hili”
“Na hatukufanya hivyo kwa sababu kamati ya maafa iliyopo ofisi ya waziri mkuu inao utaratibu wake, na kwakuwa pia kuwa watu wako mbali wanahitaji kuchangia, Katibu mkuu ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Waziri wa Nchi wameshatoa namba ya benki kuu ambayo ina ‘Contol Number’ yake ambayo wewe popote ulipo unaweza kuchangia na ikienda inakuwa tayari imehesabiwa vizuri kama ambavyo tumefanya maeneo mengine, kwahiyo mtu mwingine yeyote haruhusiwi”
“Yuko binti anaitwa Niffer nimeona anachangisha na anasema mpaka jana ameshakusanya Zaidi ya Milioni 37, atafutwe kwanza atuambie ni nani aliyempa kibali cha kuchangisha umma”