Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista J. Mhagama, Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa, pamoja na Wakuu wa Vyombo vya ulinzi na Usalama wamefika katika kijiji cha Gendabi kata ya Gendambi Wilaya ya Hanang mkoani Manyara eneo yalipotokea mafuriko ambayo yamesababisha vifo vya watu, majeruhi na uharibifu mkubwa wa Miundombinu mbalimbali, yakiwamo mashamba na makazi ya wananchi, Leo tarehe 04 Disemba 2023
Viongozi hao wameongozwa na Mkuu wa Mkoa Manyara, Queen Sendiga kufika katika Kijiji cha Gendabi ambalo ni eneo lililoathirika sana na Maporomoko ya Matope kutoka Mlima wa Hanang yaliyotokea usiku wa kuamkia tarehe 03 Disemba 2023.
Akiwa eneo la tukio hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista J. Mhagama, amewaomba wananchi hao kupokea pole ambazo zinatoka kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ambaye aliagiza lazima kufika eneo la tukio na kuona nini kifanyike kwa dharura kuhusu uokoaji pamoja na makazi kwa waathirika hao.
“Mambo haya yakitokea kuna mambo ya haraka yanatakiwa yafanyike kwa dharura hivyo tumekuja na kushauriana namna ya kujipanga kwa pamoja ili kufanikisha jambo hilo kwa uharaka” ameongeza Mhagama.
Ameongeza kuwa, maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwanza kuona namna gani tunaweza kuendelea kuokoa watu na kazi hiyo wanaendelea nayo vikosi vya uokoaji, pia kuangalia namna gani ya kuweza kuwasitiri wenzetu waliotangulia mbele ya haki.
Aidha, Waziri Mhagama amesema kuwa Serikali imeshaleta wataalamu wa Miamba watatoa taarifa ya nini kilichotokea na nini kidanyike katika mlima wa Hanang
Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema kazi ya kufungua miundombinu ya barabara inaendelea ili kurahisia kazi za uokoaji na kufikisha huduma muhimu za kijamii katika meneo yaliyoathirika.
Amesema Wakala wa Barabara nchini ( TANROADS) tayari wamefingua Barabara ya Singida-Babati ambayo awali ilikuwa haipitiki kutokana na kujaa tope na magogo ya miti kutoka milimani.