Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, amehimiza utendani makini utakaongeza ufanisi katika Mfuko wa Pensheni za Mashirika ya Umma (PPF) nchini.
Dk. Mgimwa alitoa changamoto hiyo katika hafla ya uzinduzi rasmi wa Bodi ya mpya ya Wadhamini wa PPF, Dar es Salaam, hivi karibuni.
“Cha muhimu ni kuhakikisha kuwa Bodi inazingatia kuwa kazi yake ni usimamizi na mnaiachia Menejimenti uhuru wa kufanya kazi za kiutendaji za kila siku,” alisema na kuendelea:
“Ni matarajio yetu kuwa PPF itaendelea kupata mafanikio zaidi… Haya ni matarajio ya wanachama wenu pia ili waweze kunufaika na mafao zaidi ambayo yatapatikana iwapo mtasimamia vizuri Menejimenti ya Mfuko katika utekelezaji wa mipango na malengo mtakayojiwekea.”
Alisema Serikali kupitia Wizara ya Fedha, itaendelea kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu ya Bodi hiyo ili Mfuko huo uzidi kuwa endelevu na kutoa huduma nzuri na mafao bora kwa wanachama wake.
Aidha, Waziri Mgimwa alieleza kufurahishwa na ongezeko la idadi ya wanachama wa PPF, michango inayokusanywa kutoka kwa wanachama na mapato yanayotokana na uwekezaji huo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi mpya ya Wadhamini wa PPF, Adolf Mkenda, aliahi kuwa Bodi hiyo itasimamia kuhakikisha Mfuko huo unaendeshwa kwa mujibu wa Sheria na Sera zilizopo kwa manufaa ya jamii.
Pamoja na mambo mengine, Bodi ya Wadhamini wa PPF ina majukumu ya kuhakikisha kuwa michango inakusanywa kutoka kwa wanachama kwa wakati, inawekezwa katika sehemu salama zenye riba nzuri na Mfuko huo unalipa mafao ya wastaafu kwa wakati.