……Awaandalia futari wadau wa mazingira
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni amewahimiza watanzania kutumia nishati safi kupikia kama mkakati bora wa kupambana na mabadiliko ya tabia nchi, uhalibifu wa mazingira na kuhifadhi viumbe hai.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam wakati wa futari aliyoiandaa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC kwa wadau mbalimbali.

“Tunapohimiza kuhusu mazingira hatufanyi haya yote kwa ajili yetu wenyewe, bali kwa vizazi vitakavyokuja baada yetu kwa maana ya watoto na wajukuu zetu. Ni muhimu tuendelee kushirikiana, kufanya kazi pamoja, na kufanya maamuzi ya pamoja ambayo yananufaisha mazingira na watu wanaoyategemea mazingira ambao kwa ujumla ni sisi wenyewe,” alisema.
Alisema wadau mbalimbali wanawajibu wa kutengeneza dunia endelevu na yenye maelewano kwa wote huku akisisitiza umuhimu wa kulinda rasilimali zilizopo kwa kuhakikisha zinaendelea kuwepo kwa ajili ya watoto na vizazi vijavyo.
Alisema kila mtu anatakiwa kuzingatia jinsi matendo yake , hata yawe madogo kiasi gani katika uhifadhi wa mazingira, yanaweza kuwa na athari kubwa sana kwa mazingira.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Immaculate Semesi alisema kazi inayofanywa na wadau mbalimbali katika kuhifadhi, kulinda na kusimamia mazingira ni faida kubwa kwa mazingira katika kutimiza maandiko ya vitabu vitakatifu.
“ Sote tunajua Tanzania imebarikiwa kuwa na maliasili na mifumo ikolojia ya kipekee ambayo ni pamoja na aina nyingi za mimea, wanyama, wadudu, ndege, kwa pamoja tunatakiwa kuhakikisha tunapunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kudhibiti shughuli za kibinadamu zinazoharibu mazingira kama uchimbaji madini , ufugaji na kilimo visivyo endelevu na, ukataji mkubwa wa misitu,” alisema.
Alisema juhudi za pamoja ni kuhakikisha kwamba, aina hizo tofauti za uharibifu zinapunguzwa ama kumalizwa kabisa na kwamba hilo ndilo lengo ambalo serikali kupitia NEMC inajitahidi kufikia.
Dk Semesi pia alizungumzia Siku ya Kimataifa ya Kuondoa taka (International day of zero waste) ambapo NEMC inaandaa kuaidhimisha kuanzia tarehe 28 hadi 30 Machi, 2025.

Alisema tukio hili lililopangwa kufanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar Es Salaam ni mahususi kwa kuyaleta pamoja makundi mbalimbali ya wadau wa mazingira kwa lengo la kuangazia umuhimu wa usimamizi endelevu wa taka na kukuza uchumi mzunguko (promote a circular economy).
Alisema kauli mbiu ya mwaka huu inasema “kufikia lengo la taka sifuri katika masuala ya mitindo na nguo” (“towards zero waste in fashion and textiles”) na kauli mbiu ya Kitaifa ni “TAKA NI FURSA”.
“Hii itakuwa ni fursa nyingine nzuri kwetu sote kukutana tena na kuendelea kuimarisha ushirikiano wetu katika kutafuta suluhisho la pamoja la changamoto za kimazingira zinazotukabili,” alisema.

Alisema mbali na jitihada zinazofanywa, Serikali imepiga hatua katika kuhakikisha mazingira yanalindwa na yanahifadhiwa vizuri ili kuendelea kutoa huduma na bidhaa zinazohitajika kwa kufanya tathmini ya athari za kimazingira na kijamii.
Alisema serikali imeweka mikakati mbalimbali kuhakikisha sheria za mazingira na kanuni zake zinazingatiwa na wale wanaokiuka wanaadhibiwa kwa mujibu wa sharia zilizopo.
Alisema wanafanya tafiti za mazingira na usimamizi wa maeneo maalum, kusaidia uhamasishaji na programu za kuelimisha umma na kwa kutambua kuwa mazingira ni suala mtambuka, majukumu ya usimamizi wa mazingira yanatakiwa kutekelezwa na takriban kila sekta kupitia sheria, kanuni, mikakati na mipango ya kisekta.
