Na Mwandishi Wetu, JamuhuriMedia, Zanzibar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki January Makamba (Mb) ameongoza Mkutano wa faragha wa Mawaziri wa Mambo ya Nje na wanaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki katika Jumuiya ya Afrika Mashariki unaofanyika Zanzibar.

Akizungumza katika Mkutano wa siku tatu Zanzibar ulioanza tarehe 6 na utahitimishwa Julai 8 ,2024 ambapo yeye ndiye aliyekuwa mwenyekiti,Makamba amesema Tanzania imejidhatiti kuhakikisha Jumuiya ya Afrika Mashariki inakuwa imara, yenye umoja na inayofikia malengo yakeiliyojiwekea .

“Madhumuni ya mkutano huu ni kuifanya familia yetu Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa imara, kuifanya na kutekeleza majukumu yake vizuri hivyo Tanzania nchi miongoni mwa waanzilishi wa Jumuiya hii tumejidhatiti kuona jumuiya ikiwa na umoja, imara na yenye kufanikiwa” alisema Mhe. Makamba

Naye Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Musalia Mudavadi ameipongeza Tanzania kwa kukubali kuwa mwenyeji wa mkutano huo na kuongeza kuwa ni wakati muafaka kwa nchi wanachama kuhakikisha wanatumia fursa mbalimbali ndani ya jumuiya kwa manufaa ya wananchi.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Afrika Mashariki wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Rebecca Kadaga ameipongeza Tanzania kwa juhudi zake za kuimarisha umoja wa jumuiya hiyo na kukubali mkutano huo kufanyika nchini kwake.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri Mhe. Deng Alor Kuol amesema kufanyika kwa mkutano huo ni jambo jema hasa ikizingatiwa kwa kuangalia masuala ya amani, usalama na mtangamano wa jumuiya kuifanya jumiya hiyo kusonga mbele.

Mkutano huo wa faragha uliondeshwa na Viongozi Wakuu wa nchi Wanachama wa Jumuiya kutoa taarifa na kujadili hali ya amani, usalama, siasa na uhusiano kati ya nchi wanachama; kutathmini na kujadili mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na masuala yanayokwamisha ufikiwaji wa malengo ya programu na miradi inayopangwa.

Please follow and like us:
Pin Share