Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Katavi awachunguze watumishi wawili akiwemo Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Mazingira Mpanda (MUWASA), Hussein Nyemba kwa tuhuma za kukiuka taratibu za manunuzi ya umma.
Mwingine ni Afisa Mipango Miji wa Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika, Abraham Casto ambaye anadaiwa kujipatia ardhi katika vijiji mbalimbali bila ya kufuata taratibu za kisheria na kusababisha migogo ya ardhi baina yake na wana vijiji. Watumishi wote hao wawili wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo jana (Jumatatu, Desemba 12, 2022) alipozungumza na watumishi wa Halmashauri za Mpanda, Nsimbo na Tanganyika katika ukumbi wa Mpanda Social Hall akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa mkoani Katavi. Amewasisitiza watumishi wa umma kuwatumikia wananchi ipasavyo.
Pia Waziri Mkuu ameiagiza TAKUKURU ichunguze ununuzi wa pikipiki 30 zilizonunuliwa Jijini Dar es Salaam kwa gharama ya sh. milioni 3.8 kila moja huku wilayani Mpanda pikipiki moja inauzwa sh. milioni 2.7, pia ununuzi wa mita za maji 1,000 uliofanywa bila ya kukaguliwa na TBS pamoja na ajira ya watumishi 25 alizoajiri bila kibali.
“Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema hatomvumilia mtumishi yeyote ahakikishe anasimamia majukumu yake. Watumikieni wananchi bila ya kuwabagua, sisi ni wahudumu wa wananchi lazima tufanye kazi na pangeni muda wa kuwafuata katika maeneo yao na kusikiliza kero zao na kushirikiana nao katika kuzipatia ufumbuzi.”
Kadhalika, Majaliwa ametumia fursa hiyo kumuagiza Mkuu wa Mkoa wa Katavi ahakikishe Idara ya Ardhi kuanzia ngazi ya mkoa hadi wilayani inasimamiwa vizuri. “Idara ya ardhi mkoa ijitathmini migogoro ni mingi na haishughulikiwi ipasavyo. Wananchi wana migogoro mingi ya ardhi.”
Majaliwa ametoa agizo hilo ikiwa ni utekelezaji wa maagizo Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Ndugu Abdulrahman Omari Kinana aliyoyatoa alipokuwa katika ziara ya kikazi mkoani Katavi tarehe 25 Julai, 2022. Miongoni mwa maagizo aliyoyatoa ni pamoja na kuitaka idara ya ardhi mkoa wa Katavi itazamwe kutokana na kugubikwa na rushwa na ujanja ujanja.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewaagiza wakuu wa Idara katika Halmashauri kwa kushirikiana na Madiwani waibue vyanzo vipya vya mapato na wahakikishe wanafahamu kiasi cha fedha kinachokusanywa katika kila eneo badala ya kuweka makadirio
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa muda wa mwezi mmoja kwa watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika ambao wanaishi katika Halmashauri ya wilaya ya Mpanda wakiwemo baadhi ya wakuu wa Idara wawe wamehamia Tanganyika ifikapo Januari 15, 2023 ili waweze kuwahudumia wananchi ipasavyo.
Pia, Waziri Mkuu ameagiza mkataba wa mradi wa kuzalisha hewa ukaa ambao unahusisha misitu ya vijiji vinane yenye ukubwa wa hekta 216,944 za ardhi na wakazi 34, 242 katika wilaya ya Tanganyika ukafanyiwe uchunguzi kwa mwanasheria ikiwa ni pamoja na kupitia masharti yaliyowekwa.