Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuunga mkono juhudi za kurejesha hali ya amani na usalama zinazoendelea kufanywa sehemu mbalimbali barani Afrika ikiwemo Ukanda wa Afrika Magharibi, Pembe ya Afrika na Sudan Kusini.
Waziri Kombo ameeleza hayo alipokuwa akihutubia Mdahalo wa Kwanza wa Amani na Usalama Afrika (APSD) uliolenga kujadili na kupata ufumbuzi wa migogoro inayoendelea sehemu mbalimbali barani Afrika ulioandaliwa na Taasisi ya Thabo Mbeki, uliofanyika jijini Johannesburg, nchini Afrika Kusini terehe 6 Oktoba 2024.
Tanzania tukiwa wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika tunaunga mkono juhudi zote zinazofanywa na Jumuiya za Kikanda, Kimataifa na Taasisi mbalimbali ili kurejesha amani na usalama katika maeneo husika, Afrika tumejaliwa utajiri wa rasilimali tuache migogoro. Ameeleza Waziri Kombo
Waziri Kombo akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mdahalo huo, mbali na kuunga mkono juhudi ametoa wito kwa wadau wa amani kote Afrika kuhakikisha kuwa pande zote zinazohusika kwenye migogoro sehemu mbalimbali barani, zinahusishwa katika kila hatua ya utatuzi wa migogoro hiyo ikiwemo kualikwa kwenye mazungumzo na midahalo ya kujadili masuala ya amani na usalama.
Akielezea kuhusu mchango na uzoefu wa muda mrefu wa Tanzania katika masuala ya ujenzi wa amani na usuluhishi wa migogoro sehemu mbalimbali barani Afrika, Waziri Kombo amehimiza umuhimu wa kushirikisha Wanawake na Vijana kwenye shughuli za kulinda na kurejesha amani na usalama.
Aidha, Waziri Kombo kwenye mdahalo huo amebainisha masuala mengine saba (7) muhimu ya kuzingatiwa kwenye juhudi za kulinda amani na usalama barani Afrika, ambayo ni kuimarisha ushirikiano na wadau wa kikanda na kimataifa katika kutafuta rasimalimali na utalaamu unaohitajika kwenye utatuzi wa migogoro husika, kuhakikisha mazungumzo ya kutafuta amani na usalama yanakuwa jumuishi, kuzingatia utawala bora, demokrasia na haki za binadamu na kuwawezesha Wanawake na Vijana.
Masuala mengine ni kuwekeza katika kuimarisha mtangamano wa kikanda, kuimarisha mifumo ya kuonesha viashiria vya uvunjifu wa amani na usalama, ikiwemo uhalifu katika maeneo ya mipakani na kuwekeza katika kujengeana uwezo zaidi kwenye masuala ya amani na usalama.
Kwa sasa Tanzania inachangia vikosi vya kulinda amani na usalama katika maeneo mbalimbali ikiwemo Afrika ya Kati, Jumhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Msumbiji katika jimbo la Cabo Delgado na Sudani Kusini.