Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo amewakaribisha wafanyabiashara wa Czech kuangalia fursa za uwekezaji nchini Tanzania katika sekta za utalii uchukuzi, afya, TEHAMA, nishati, madini na elimu.

Waziri Kombo alitoa mwaliko huo alipofanya mazungumzo na wamiliki na viongozi wa kampuni kubwa za Czech wakati wa ziara yake ya kikazi aliyoifanya nchini humo kuanzia tarehe 16 hadi 18 Januari 2025.

Alisema Czech ni nchi iliyopiga hatua kubwa ya maendeleo katika sekta mbalimbali, hivyo Tanzania ina fursa kubwa ya kunufaika kwa uhaulishaji wa teknolojia na mitaji katika sekta mtambuka na watanzania wakafaidika kwa kupata ajira na ujuzi.

Waziri Kombo aliwaambia wafanyabiashara hao kuwa Mungu ameiweka Tanzania katika eneo la kimkakati na kuipa utajiri mkubwa wa rasilimali. Hivyo, hawatajuta, wakiichagua Tanzania kuwekeza mitaji yao kwa kuwa uhakika wa soko ni mkubwa ukizingatia kuwa Tanzania ni mwanachama wa EAC, SADC na sasa Soko Huru la Biashara barani Afrika.

Maeneo ambayo Mhe. Waziri Kombo amekuwa akipendekeza kwa wafanyabiashara hao ni pamoja na miradi ya ujenzi wa boti kwa ajili ya kukuza uchumi wa buluu na kuimarisha miundombinu ya majini visiwani Zanzibar, kuwekeza katika miradi ya kuzalisha nishati ya umeme na miradi ya nishati safi ya kupikia ili kufikia mpango wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha kuwa ifikapo 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia, na kuwa na miradi ya ubia ya kuongeza thamani bidhaa za Tanzania ili ziweze kushindana na kukidhi vigezo vya soko la nje na ndani ya nchi.

Maeneo mengine ni sekta ya afya ambapo Tanzania inaweza kunufaika kwa kupata mafunzo ya watalaamu wake na vifaa vya kisasa vya tiba kufuatia Czech kuwa na maendeleo makubwa kwenye eneo hilo. Aidha, eneo la uchukuzi limesisitizwa sana na Mhe. Waziri Kombo hasa ushirikiano katika anga, reli, bandari na mpangilio (logistic). Aliipongeza kampuni ya SKODA kwa mchango wake wa kuweka mfumo wa umeme katika reli ya SGR.

Kwenye ziara hiyo ya siku tatu nchini Czech, Mhe. Waziri alipata fursa ya kukutana na Kampuni zaidi ya 10, kuongea na viongozi wake na nyingine kuzitembelea katika karakana zao. Kampuni hizo ni pamoja na EP Cargo, Ostava Airport, PAMCO International, AOT, CZECH railway, CHLAD, SKODA, UJP PHARA, HAVEL & PARTNERSS na TATRA.