Katika kipindi cha mwezi mmoja sasa, Watanzania wameshuhudia sakata la Kampuni ya Lugumi iliyopata tenda Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Kutokana na sakata hili kushika kasi, tumeweza kuona jinsi mkataba huo unavyosumbua viongozi wetu kimyakimya, huku Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, akitajwa katika sakata hilo kupitia Kampuni ya Infosys.
Waziri Kitwanga anatajwa kuhusika katika kashfa hii kubwa ndani ya Jeshi la Polisi akiwa ni waziri wa wizara inayoongoza Jeshi la Polisi – kashfa ya ufisadi wa shilingi billion 34.
Jeshi la Polisi limekumbwa na kashfa ya ununuzi wa vifaa vya kuhifadhi alama za vidole ambapo kampuni ya Infosys inayohusishwa na Waziri Kitwanga ni moja ya kampuni zilizonufaika na mkataba huo.
Kutokana na kuibuka huko kwa sintofahamu kati ya Waziri Kitwanga na kampuni hiyo inayoelezwa kuhusika naye, Kitwanga ni waziri wa kwanza katika Baraza la Mawaziri wa Awamu ya Tano, wateule wa Rais Dk. John Magufuli kukumbwa na kashfa.
Kutokana na kaulimbiu ya Rais wetu mwenye msimamo, nilitaraji kuona waziri huyu wa Mambo ya Ndani akiachia wadhifa wake kwa kujiuzulu. Kitwanga ana wajibu wa kuachia madaraka yake kutokana na kashfa hii. Ni vyema kuwajibika kwake maana anaongoza wizara ambayo anaelezwa kuwa na mgongano wa maslahi.
Falsafa ya Rais wetu ni kuwa anataka viongozi wasafi wasio na chembe ya uovu katika utendaji kazi wa kila siku. Kitwanga siyo msafi tena wa kuweza kwenda na kasi ya Rais wetu kutokana na kashfa hii.
Ili kulinda heshima yake na heshima ya Baraza la Mawaziri wa Rais wetu mzalendo, ni busara sasa kwa waziri wetu huyu kukaa kando na kumpatia Rais nafasi ya kufanya uteuzi mwingine katika nafasi hiyo.
Hii yote ni kutokana na kumpatia Rais fursa ya kutimiza wajibu wake kwa kuwa na watu wasiotiliwa mashaka pamoja na kurudisha nidhamu ya kazi.
Tanzania ya sasa inataka kuona viongozi walio tayari kuwajibika pale wanapohitajika kufanya hivyo. Uongozi ni dhamana, siyo lazima kuendelea kung’ang’ania kubaki katika ukubwa unaotiliwa shaka.
Kila siku Rais wetu anakutana na changamoto ya baadhi ya viongozi wanaodaiwa kutumia vibaya madaraka yao. Kwa hili la Kitwanga wala halihitaji kutumia nguvu kubwa bali ni yeye mwenyewe kuomba ‘po’ na kuwaacha wenzake waendeleze gurudumu la Tanzania tuitakayo.
Natambua ya kuwa Kitwanga ni muungwana na ana nia njema kabisa ya kumsaidia Rais wetu katika kuboresha maisha ya Watanzania. Na atakuwa tayari amefanya uamuzi wa kuachia nafasi yake ya uwaziri lakini bado anatafakari.
Hivyo basi, nachukua fursa hii kumkumbusha ya kuwa wakati sasa umefika wa kufanya uamuzi sahihi wa kujiuzulu nafasi hiyo na kubaki kuwa mshauri wa Rais akiwa nje ya Baraza la Mawaziri kama wengine wanavyofanya.
Kwa jinsi ninavyomfahamu Waziri Kitwanga, sidhani kama anasubiri Rais amtumbue.