Na Mwandishi Wetu

NAIBU Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete amemuelekeza Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Manyara kuweka mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi na kuwapatia hati wakazi wa eneo la ekari 2,390 zilizotolewa na Rais katika Bonde la Kiru Wilaya ya Babati mkoani Manyara.

Kikwete alitoa maelekezo hayo kwa Kamishna Joseph Batinamani wakati alipofanya ziara Februari 11, 2023 katika kijiji cha Kiru Dick kata ya Kiru,Halmashauri ya Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara, kutokana na mgogoro uliopo kati ya wakazi wa Kijiji cha Kiru Dick Valley na mwekezaji wa kampuni ya Hamir Estate Ltd inayojishughulisha na kilimo cha miwa ambaye ni wamiliki wa awali wa Mashamba hayo.

Itakumbukwa kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan aliamua kumega ekari 2,390 ambazo zilikuwa zikimilikiwa kihalali na Kampuni ya Hamir Estate Ltd kwenye mwaka 1999 na kuwapa wananchi ili kumaliza mgogoro huo.

Wananchi hao mpaka sasa bado hawajakabidhiwa maeneo hayo kwa kuwa bado Serikali inafanya mazungumzo na mwekezaji huyo kuhusu fidia ili kuachia maeneo hayo yaende kwa wananchi.

Aidha Kikwete amewaonya wakazi wa eneo hilo kujiepusha na uvunjifu wa amani kwa kujihusisha na vitendo vya kihalifu ambavyo vimekuwa vikiendelea katika eneo hilo na badala yake amewataka kuonesha ushirikiano kwa muwekezaji huyo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Manyara Charles Makongoro Nyerere amewataka wakazi wa eneo hilo kuwa nasubira wakati Serikali ikiendelea na utekelezaji wa maelekezo ya Rais ili wananchi hao waweze kupangwa na kumilikishwa maeneo hayo na kupatiwa hati za umiliki wa ardhi Kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo wananchi hao walipewa nafasi ya kuzungumza ambapo waliiomba Serikali ishughulikie suala hilo haraka.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete Pamoja na mkuu wa Mkoa Manyara Charles Makongoro Nyerere walilazimika kuanza kutoa darasa kwa wananchi hao juu ya taratibu zote za ardhi kwa zaidi ya saa tatu.

Bonde la Kiru ni eneo la bonde la ardhi lenye rutuba kuliko eneo lolote la kilimo katika Mkoa wa Manyara linalopatikana katika Wilaya ya Babati Vijijini takribani kilomita 12 kutoka Babati Mjini njia ya Babati -Arusha.

Kutokana na eneo hili kuwa na rutuba sana limevutia wawekezaji wakubwa wengi wa kigeni na wenyeji wachache kwenye shughuli za kilimo hasa kilimo cha miwa toka enzi za Mjerumani na baadae Muingereza pamoja na mataifa mengine kama Urusi, Swedeni, Marekani toka miaka ya 1930.

Kuanzia mwaka 1968 mpaka miaka ya mwanzoni ya 1970 Serikali ilitekeleza sera ya uanzishwaji wa Vijiji vya Ujamaa ambayo ilipelekea kuanzishwa kwa Vijiji vya Ujamaa ndani ya baadhi ya mashamba haya ya wawekezaji katika Bonde la Kiru ambayo yalikuwa yamevamiwa na hayajaendelezwa.

Hali hii ilipelekea kuibuka kwa migogoro mingi ya ardhi katika Eneo la Kiru Valley baada ya Serikali kutambua na kusajili baadhi ya Vijiji ndani ya mashamba kutokana na uhitaji mkubwa wa ardhi uliokuwepo kipindi hicho.

Ili kutatua migogoro hii ilionekana ni bora kufuta umiliki wa mashamba haya ili mashamba haya yarejeshewe kwa wananchi ambao ni wakazi wa Kijiji cha Kiru Dick Valley.

Hata hivyo baada ya Serikali kuchukua hatua ya ufutaji wa mashamba haya na kuwagawia wananchi bado hatua hiyo haikuweza kumaliza mgogoro huu wa ardhi kwani baadhi ya wanavijiji waliendelea kutaka ardhi zaidi hali iliyoendelea kuleta mvutano ya miaka mingi baina ya wawekezaji waliokuwa na mashamba hayo.

Hali hii ya mivutano iliendelea na hali ilikuwa mbaya zaidi ambapo mwaka 2011 kulitokea uvunjifu wa amani (vurugu) zilizosababisha uharibifu wa mazao, vifaa, makazi na hatimaye maisha ya mlinzi wa shamba la Kiru Valley Estate.