Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dkt.Ashatu Kijaji ,ameeleza ujenzi wa viwanda na kongani za kutosha nchini utasaidia kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana wa kitanzania ambao wanamaliza masomo yao kila mwaka zaidi ya milioni moja kutoka vyuo mbalimbali.
Aidha ameeleza ,Serikali inaendelea kushirikiana na sekta binafsi ili kuinua uwekezaji pamoja na kukuza uchumi wa Taifa letu.
Hayo aliyaeleza wakati alipotembelea kongani ya kisasa ya viwanda Modern Industrial Park ,Disunyara ,Mlandizi Kibaha, mkoani Pwani (KAMAKA) ,kujionea utekelezaji unavyoendelea na kuona changamoto zilizopo ili kuzibeba na kwenda kuzifanyia kazi kupitia mawaziri wa kisekta.
Kijaji alifafanua kwamba , kuna kila sababu ya kuwatengenezea vijana hao mazingira ya ajira za kuajiriwa na kujiajiri .
“Muunganiko wa viwanda ,utasaidia kuongeza ajira za kutosha, na hiyo inajiidhihirisha katika kongani hii ambayo kutatengeneza ajira za moja kwa moja 30,000 .”
“”Tanzania ilishaamua tuliposema tunataka mapinduzi manne ya viwanda ,tulisema atutaki kuachwa nyuma tangu tulipotengeneza dira yetu ya maendeleo ya Taifa miaka 24 iliyopita mwaka 2000 ambayo tutaikamilisha 2025”
“Na Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani alieleza dhamira yake ya ujenzi wa uchumi wa Taifa letu kuuacha mikononi mwa sekta binafsi ,Hakuna Taifa lililoendelea bila kwenda na sekta binafsi iliyowezeshwa na ameendelea kutenda kwa vitendo kwa kusafiri na watu wa sekta binafsi ili kuwakutanisha na wawekezaji nje ya nchi”alisisitiza Kijaji.
Kijaji alimpongeza mwekezaji huyo wa ndani ,KAMAKA Co.Ltd kwa kuthubutu na kuwa na utayari kwa uwekezaji huo mkubwa.
Kuhusu changamoto za kongani hiyo ,Kijaji alisema zipo ambazo zimeanza kufanyiwa kazi na ameibeba changamoto ya uhitaji wa barabara ya kiwango cha lami kutokea Mlandizi ili iweze kufungua uchumi na kuvutia wawekezaji.
Alieleza, atakaa na waziri wa ujenzi Innocent Bashungwa ili kuangalia namna ya kufanikisha ombi hilo .
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alieleza barabara ya kuanzia Makofia -Mlandizi -Mzenga -Vikumburu -Mloka ni muhimu kwani inapitia eneo la uwekezaji na miradi ya kimkakati.
Kunenge aliomba wakati ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami ukianza ,uanzie Mlandizi kwa maslahi mapana ya eneo hilo.
Mkuu huyo wa Mkoa alieleza ,kuhusu Changamoto ya maji alishaongea na waziri wa maji Jumaa Aweso na ameahidi kufika kwenye kongani hiyo kujionea uhalisia wa tatizo.
Awali Ofisa Fedha na Masoko kutoka KAMAKA Co.Ltd Tumaini Kabengula, alieleza kongani hiyo itakapokamilika itatoa ajira 200,000 na za moja kwa moja 30,000.
Kuhusiana na hatua ya utekelezaji , alieleza wamefikia asilimia 93 katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa miundombinu ambao utakamilika mwezi Februari mwaka huu .
Kabengula alisema ,mradi huo unatarajia kugharimu trilioni 3.5 kati ya fedha hizo bilioni 122.4 zitajenga miundombinu ndani ya kipindi cha miaka mitano ambapo hadi sasa sh .bilioni 35 zimetumika kwa ujenzi wa miundombinu na gharama zinazohusiana na uwekezaji huo.
“Mradi ulianza kutekelezwa oktoba 2021 ,kwa awamu ya kwanza kwenye ujenzi wa lango kuu na uzio,kituo cha polisi,jengo la utawala,ofisi na jengo la makazi ya wafanyakazi wa zimamoto,zahanati,kituo cha umeme wa megawatt 54 ,mfumo wa barabara za nje na ndani na umefikia asilimia 93” alibainisha Kabengula.
Mkurugenzi Mtendaji, Mkandarasi Mkuu Afriq Engineering and Construction Co.Ltd Charles Bilinga alieleza wanakabiliwa na changamoto ya umeme na miundombinu wezeshe ikiwemo barabara kiwango cha lami.
Alitaja changamoto nyingine ni Changamoto utoaji wa vivutio vya kodi kwa kongani jirani na kutokuwepo vivutio hivyo katika kongani ya Modern Industrial Park licha ya uwekezaji mkubwa uliofanyika na unaoendelea kufanyika kuna haribu ushindani wa haki wa kibiashara.
“Baadhi ya wawekezaji wanashindwa kuchukua viwanja ndani ya kongani kwasababu ya kukosekana kwa vivutio vya kikodi kama ambavyo vinapatikana katika kongani jirani.