Na Magrethy Katengu,JamuhuriMedia
Dar es Salaam

Waziri wa Maliasili wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki (Mb) ametoa wito kwa nchi wanachama wa mkakati wa kuokoa ardhi na misitu iliyoharibiwa takribani Hekta milioni 100 Barani Afrika (African Forest Restoration Initiatives – AFR100) kwa kuweka mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ya kielektroniki kuhakikisha lengo la linafikiwa ifikapo 2030 kuona uhalisia halisi.

Yamebainishwa hayo leo Juni 21,2024 jijini Dar es Salaam katika Mkutano wa 8 wa Mwaka wa nchi 34 za Afrika Wanachama katika Mkakati wa Uokoaji wa Ardhi na Misitu iliyoathiriwa miaka yq nyuma kutokana na shughuli za binadamu ikiwemo ukataji miti, uchomaji mkaa.

“Ni muhimu kuweka mikakai na mifumo ya ufuatiliaji na urejeshaji wa misitu na uwajibikaji ili tuweze kuona hali halisi ya kinachoripotiwa katika maeneo husika kuhusu urejeshaji wa misitu” Mhe. Kairuki amesisitiza na kuongeza kwamba Tanzania imeanza kuangalia namna ya kuweka mfumo hiyo ili kuweza kufuatilia, kurahisisha upatikanaji wa taarifa”amesema Waziri

Kairuki Ameongeza kwa kusema kuwa katika kutekeleza mpango huo wa kurejesha misitu, Tanzania imefanikiwa kurejesha hekta milioni 2.4 kupitia afua za upandaji miti, ambayo ni sawa na asilimia 46.3 ambapo iliahidi kurejesha hekta milioni 5.2 za misitu na mandhari kwa mwaka 2018.

“Ili kudhihirisha nia thabiti ya Serikali ya utekelezaji wa mkakati wa kuongoa misitu nchini, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliongoza kampeni ya upandaji miti katika siku yake ya kuzaliwa mwaka 2023 kijijini kwao Kizimkazi Zanzibar ambapo zaidi ya miti 1,500 ilipandwa katika siku hiyo, lakini kampeni ya upandaji miti iliendelea kwa mwezi mzima ambapo miti takribani milioni 8.3 ilipandwa” Mhe. Kairuki aliweka bayana.

Amesema kuwa Rais Samia amekuwa kinara Barani Afrika na duniani katika kuhakikisha misitu inaongolewa na kutunzwa hasa kupitia kampeni yake ya nishati safi ambapo ameendelea kuhamasisha nchi nyingine duniani kutoa ahadi za kuhakikisha zinalinda misitu na zinaweka afua mbalimbali za kulinda misitu.

Kwa upande wake Kamisha wa Uhifadhi wa Misitu Tanzania Prof.Dosantos Silayo amesema Dunia imeweka lengo la kukomboa ardhi ya Tanzania katika kuchangia utunzaji wa mazingira ikiwemo misitu.

Aidha amesema Dunia imeweka lengo la kukomboa Milioni 350 ambapo kwa nchi za Afrika wameweka lengo la kulinda hekta takribani Milioni 100.

Hata hivyo amesema Tanzania katika kuhakikisha kuwa inakomboa ardhi ikiwemo misitu imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa marekebisho ya sera, sheria na kanuni katika kutunza rasilimali za misitu.

Aidha Mkutano huo umehudhuriwa na wawakilishi kutoka zaidi ya Nchi 34 Wanachama wa Afrika na Taasisi za Kifedha wanaojishughulisha na AFR100. Mkakati huo ulianzishwa Desemba 2015 ili kushughulikia changamoto za kimazingira, kiuchumi na kijamii zinazoathiri usimamizi wa maliasili Barani Afrika kwa lengo la kurejesha zaidi ya hekta milioni 100 za misitu iliyokatwa na kuharibiwa ifikapo mwaka 2030.

Please follow and like us:
Pin Share