Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Japan hapa nchini, Mhe. Yasushi Misawa katika Mji wa Serikali, Mtumba Jijini Dodoma.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika leo Septemba 14, 2023 Dkt. Jafo amemshukuru Balozi Misawa kwa juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Japan kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo (JICA) kwa kuendelea kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo maji, elimu, barabara, afya na kuiomba Serikali hiyo kusaidia pia miradi ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira iliyopo nchini.
Waziri Jafo amemueleza Balozi Misawa kuwa ajenda ya mazingira ni moja ya kipaumbele muhimu vilivyopewa msukumo na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea na juhudi za kuhamasisha jamii kutumia nishati mbadala ili kuhamasisha uhifadhi na utunzaji mazingira nchini.
“Tanzania tunazalisha takribani tani Milioni moja za taka ngumu ambazo ni fursa ya uzalishaji wa nishati mbadala…tunatumia asilimia 30 tu ya nishati hiyo…Tunahitaji nishati hii kwa ajili ya matumizi ya kijamii na kiuchumi. Tunahitaji wawekezaji wengi zaidi kujitokeza kwa ajili ya uwekezaji,” amesema Mhe. Dkt.Jafo.
Amesema kuwa Serikali imeweka mazingira wezeshi na rafiki kwa wawekezaji na wadau wa nishati hiyo kuweza kujitokeza na kushirikiana na Serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya nishati mbadala hususani katika maeneo ya vijijini ili kuongeza upatikanaji wa nishati mbadala ya kupikia.
Waziri Jafo pia amemhakikishia Balozi Misawa ushirikiano na utayari wa Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya nishati jadidifu ikiwemo jotoardhi, tungamotaka, upepo na jua pamoja na matumizi bora ya Nishati mbadala ili kuleta manufaa kwa wananchi na jamii kwa ujumla.
Akifafanua zaidi Waziri Jafo amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa sera, kanuni na miongozo mbalimbali ikiwemo ikiwemo katazo Kwa taasisi zote za umma na binafsi kwa upande wa Tanzania Bara zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi 300 kusitisha matumizi ya mkaa na mkaa ifikapo mwaka Januari 2025.
Dkt. Jafo amesema kutokana na msisitizo huo, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imendelea kuwahimiza wadau na washirika wa maendeleo kujitokeza kuungana mkono juhudi hizo za serikali kwa kuhakikisha zinaelekeza nguvu katika uwekezaji wa miradi ya nishati Rafiki kwa mazingira.
Aidha kwa upande mwingine Dkt. Jafo ameiomba Serikali ya Japan kutoa fursa ya ufadhili wa masomo kwa wataalamu wa mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais ili kuweza kujengewa uwezo wa kitaalamu na kiufundi katika usimamizi wa miradi mbalimbali ya mazingira inayotekelezwa nchini.
Kwa upande wake, Balozi Misawa amemhakikishia Waziri Jafo kuwa Serikali ya Japan itaendelea kuwa mdau mkubwa wa maendeleo kwa kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza sekta ya Nishati hasa kwa upande wa Nishati jadidifu.
Alisema, kuwa wawekezaji kutoka Japan wapo tayari kuja kuwekeza nchini Tanzania katika sekta ya nishati jadidifu na kuhakiikisha kuwa uwekezaji huo unaleta manufaa ya kijamii na kiuchumi baina ya Mataifa hayo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo akzungumza jambo wakati wa kikao baina yake na Balozi wa Japan nchini Tanzania, Yasushi Misawa yaliyofanyika leo Septemba 14, 2023 katika Mji wa Serikali, Mtumba Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Selemani Jafo akipokea kitabu utekelezaji wa miradi ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japani (JICA) kutoka kwa Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa mara baada ya mazungumzo baina yao yaliyofanyika leo Alhamisi Septemba 14, 2023 katika Mji wa Serikali, Mtumba Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Selemani Jafo akimkabidhi nyaraka mbalimbali za taarifa kuhusu majukumu ya Ofisi hiyo Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa mara baada ya mazungumzo baina yao yaliyofanyika leo Septemba 14, 2023 katika Mji wa Serikali, Mtumba Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Selemani Jafo akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Japan Mhe. Yasushi Misawa pamoja na viongozi wengine mara baada ya mazungumzo baina yao yaliyofanyika leo Septemba 14, 2023 katika Mji wa Serikali, Mtumba Jijini Dodoma. (PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)
……………..