Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema takriban dola milioni 800 zinapotea duniani kila mwaka kutokana na wanawake kutumia muda mwingi kutafuta kuni badala ya kufanya shughuli za kuingiza kipato.
Amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Uhamasishaji wa Matumizi ya Nishati Safi kupitia Vikundi vya Akiba na Mikopo vya Vijiji (VSLAS) uliowezeshwa na Kanisa la Tag-City Light Temple Goba Matosa mkoani Dar es Salaam tarehe 27 Mei, 2024.
Dkt. Jafo amesema kuwa kutokana na takwimu hizo kuna umuhimu mkubwa wa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhamasisha jamii kutumia nishati safi ya kupikia na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa kwani ni asilimia 6.7 tu ya kaya ndio wanatumia nishati safi.
Amesema kuwa matumizi ya kuni na mkaa yanagharimu afya za watu na kwamba inakadiriwa kuwa dola bilioni 1.4 duniani kila mwaka zinatumika kuwatibu wanawake walioathirika kiafya.
Kutokana na matumizi ya nishati chafu, amesema kuwa maisha ya wakinamama hususan wenye umri mkubwa vijijini wanahatarisha maisha yao wanapotumia kuni na kuwa na machi mekundu hali inayowafanya wahisiwe ni wachawi.
Dkt. Jafo amesema Serikali imekuwa ikielekeza utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti kwa wingi kupitia kampeni mbalimbali ili kulinda afya na mazingira kwa ujumla.
Aidha, amewataka wananchi kuungano mkono maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kulega malengo ya dunia ya kuhakikisha jami inapata nishati safi ya kupikia
“Dunia yetu leo hii changamto ya uwepo wa nishati chafu ya kupikia bado ni kubwa hivyo tuna kila sababu ya kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishato safi ya kupikia,” amesema Dkt. Jafo.
Halikadhalika amewapongeza wadau wanaojitolea kufanikisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia hususan ya gesi hatua inayosaidia jamii kuweza kupata hamasa ya kutumia na kuachana na kuni na mkaa.
Kwa upande wake Askofu na Mchungaji Kiongozi wa wa Kanisa la Tag-City Light Temple Dkt. Mulenda Omary amesema wamedhamiria kuwa ifikapo mwaka 2024 jamii nchini kote iwe inatumia nishati safi ya kupikia.
Amesema kuwa kupitia VICOBA wanavikundi watawawezeshwa kununua na kujaza gesi ambayo itasaidia kuepukana na matumizi ya mkaa katika kuandaa chakula.
Awali akisoma risala, katibu wa kanisa hilo, wa Bw. Geharzberg Kaywanga amesema mpango wa uhamasishaji unakusudia kufikia malengo makuu matatu ambayo ni kuhamasisha upatikanaji mpana wa suluhisho la nishati safi kupitia vikundi vya akiba na mikopo na makundi mengine katika jamii, haswa katika maeneo ya vijijini na mijini ambako umaskini wa nishati unaendelea.